WIZARA YA AFYA YATOA TAHADHARI UWEPO WA COVID -19

Na Nora Damian, The Page

Wizara ya Afya imesema tangu Februari hadi Aprili mwaka huu kumekuwa na ongezeko la visa vya ugonjwa wa Covid -19 hasa katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Mei 20,2025 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe, hali ya kuongezeka na kupungua kwa ugonjwa huo imekuwepo kila mwaka tangu ulipotangazwa mwaka 2020 na kwa kipindi hiki ongezeko linaonekana zaidi katika Mkoa wa Dar es Salaam.

"Ugonjwa wa UVIKO-19 ambao ulitangazwa kwa mara ya kwanza hapa nchini Machi 2020, umeendelea kuwepo kwa kiwango cha chini kama yalivyo magonjwa mengine ya mfumo wa njia ya hewa.

"Tangu Februari hadi Aprili 2025, ufuatiliaji wa virusi hivyo umeonesha ongezeko la visa vya UVIKO-19 kutoka asilimia 1.4 (wagonjwa 2 kati ya watu 139 waliopimwa) Februari hadi asilimia 16.3 (wagonjwa 31 kati ya 190 waliopimwa) Machi, na kisha asilimia 16.8 (wagonjwa 31 kati ya watu 185 waliopimwa) mwezi Aprili 2025," amesema Dk. Magembe. 

Amesema wanaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa nchini na kutoa taarifa.

"Kupitia vituo vyake vya kutolea huduma, wizara imeelekeza wataalam kuhakikisha wanaendelea kufanya utambuzi wa magonjwa haya kwa kutumia vipimo vya maabara na kutoa matibabu stahiki kwa wagonjwa wote wanaobainika kuwa na maambukizi.

"Natoa rai kwa wananchi wote kuzingatia kanuni za afya ili kujikinga na kuwalinda wengine dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa ikiwa ni pamoja na kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya pamoja na kuvaa barakoa pale inapohitajika," amesema.

Tahadhari nyingine ni kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi mara kwa mara, kudumisha usafi wa mwili binafsi na wa mazingira yanayotuzunguka.

Aidha amesema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi, hususan katika Mikoa ya Pwani kumekuwa na ongezeko la hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayoenezwa na mbu kama vile Homa ya Dengue, Malaria na magonjwa mengine ya aina hiyo. 

Mganga Mkuu huyo wa Serikali amesema ili kujikinga na madhara yatokanayo na magonjwa hayo amewasihi wananchi kuchukua tahadhari kwa kuangamiza mazalia ya mbu, kuondoa maji yaliyotuama karibu na makazi ikiwemo madimbwi, ndoo, chupa, matairi ya zamani na vifaa vingine vinavyoweza kuhifadhi maji.

Pia kutumia vyandarua vyenye dawa, kupulizia viuatilifu ndani ya nyumba mara kwa mara ili kuua mbu waliopo ndani, kuvaa nguo ndefu zinazofunika mwili hasa wakati wa jioni na alfajiri, kufunga madirisha na milango au kutumia wavu ili kuzuia mbu kuingia ndani ya nyumba.

"Magonjwa haya yanayosababishwa na virusi yana dalili zinazoshabihiana hivyo ni vigumu kuyabaini bila kupata vipimo vya maabara. Hivyo, nawasihi kuwahi katika vituo vya kutolea huduma mara mnapopata dalili zozote za homa, maumivu ya kichwa, macho, misuli, viungo, au vipele mwilini au dalili za magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa kama vile kikohozi, mafua, kuwashwa koo au kupumua kwa shida ili kupata vipimo na matibabu stahiki," amesema.

Dk. Magembe amesema pia vipimo vya maabara vimebaini kuongezeka na kupungua kwa virusi vya influenza hali ambayo imekuwa ikionekana pia katika miaka iliyopita na ndiyo maana hujulikana kama 'Seasonal influenza'.

Amesema vipimo hivyo vimeonesha kuwa hakuna kirusi kipya kinachoweza kusambaa kwa haraka na kusababisha mlipuko wa aina ya Pandemiki.





Powered by Blogger.