WANANCHI MILIONI 7 WANUFAIKA HUDUMA ZA KISHERIA TAWLA IKIADHIMISHA MIAKA 35

Na Nora Damian, The Page

ZAIDI ya wananchi milioni saba wamepatiwa huduma mbalimbali za msaada wa kisheria kupitia Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) zilizowezesha kupata haki zao na kupunguza ukatili wa kijinsia.

Chama hicho mwaka huu kinasherehekea miaka 35 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1989 na kusajiliwa rasmi mwaka 1990. 

Akizungumza leo Mei 20,2025 na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TAWLA, Tike Mwambipile, amesema wananchi hao wamefikiwa kupitia mtandao wa ofisi zake zilizopo katika mikoa mbalimbali nchini.

"Huduma hizi zimekuwa na mchango mkubwa katika kuwasaidia wanawake na watoto kupata haki zao kwa njia ya kisheria, kuimarisha uelewa wa sheria katika jamii, na kupunguza ukatili wa kijinsia," amesema Mwambipile.

Aidha amesema wamewezesha mafunzo na upitishaji wa sheria ndogo za vijiji zenye mlengo wa kijinsia katika vijiji 178 katika Mkoa wa Tanga, Mwanza, Arusha, Pwani, Morogoro, Kilimanjaro, Njombe na Mbeya lengo likiwa kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya kijamii kuhusu ardhi. 

Amesema TAWLA imewezesha takribani wanawake 400 kuweza kupata Hati milki ya kimila pamoja hati milki za ardhi 51 kwa wanawake.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali chama kimetoa mchango mkubwa katika mchakato wa maboresho ya sheria na sera kadhaa muhimu zikiwemo Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, Sheria ya Ardhi Na. 4 na 5 za mwaka 1999.

Sheria nyingine ni ile ya Mtoto ya mwaka 2009, Marekebisho ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sheria ya Mirathi na sheria nyingine zinazohusiana na masuala ya urithi, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971. 

Kuhusu masuala ya uongozi amesema katika kipindi cha miaka 35, wamefanikiwa kuwajengea uwezo wanawake zaidi ya 500 waliogombea nafasi mbalimbali za uongozi, kuanzia ngazi ya kijiji hadi ngazi ya taifa. 

"Mafanikio haya yanadhihirisha mchango wa TAWLA katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi na kutoa mchango wa maana katika ujenzi wa taifa lenye usawa na haki kwa wote," amesema Mwambipile.

Maadhimisho ya miaka 35 yameambatana na kongamano kubwa litakalofanyika Mei 22 na 23, 2025 jijini Dar es Salaam lenye lengo la kujadili kwa kina masuala muhimu yanayogusa haki za wanawake na watoto wa kike.




Powered by Blogger.