BODI YA ITHIBATI KUANZA KUSAJILI WAANDISHI WA HABARI, YAONYA WATAKAOGUSHI VYETI

Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Tido Mhando, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuanza usajili wa waandishi wa habari, Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

BODI ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imetangaza kuanza kuwasajili waandishi wa habari na kuonya kuwa watakaobainika kuwasilisha vyeti au nyaraka za kugushi watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumza leo Mei 19,2025 na vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Tido Mhando, amesema kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya vyombo vya habari kumekuwa pia na ongezeko la waandishi wa habari wanaofanya kazi katika vyombo vya habari, jambo ambalo linahitaji usimamizi wa kitaaluma ili kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi kwa kufuata maadili ya taaluma yao. 

"Kuwathibitisha waandishi wa habari ni hatua muhimu katika kuhakikisha taaluma ya uandishi wa habari inazingatia viwango vya kitaaluma, maadili na uwajibikaji. 

"Kupitia ithibati itaonyesha waandishi wa habari wenye sifa stahiki na waliopata mafunzo yanayohitajika ili kufanya kazi kwa ufanisi," amesema Mhando.Mwenyekiti huyo amesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha weledi katika tasnia ya habari na kudhibiti usambazaji wa habari zisizo sahihi na kulinda haki na uhuru wa waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao. 

Aidha ametahadharisha kuwa waandishi wa habari watakaobainika kuwasilisha vyeti au nyaraka za kughushi watachukuliwa hatua kali bila kujali hatua waliyokuwa wamefikia katika mchakato wa usajili.

"Hatua hizi zitajumuisha kufutiwa mara moja usajili wao, kuwasilishwa katika vyombo vya sheria kwa ajili ya kuchukuliwa hatua stahiki, pamoja na kupigwa marufuku kujihusisha na shughuli za uandishi wa habari au majukwaa mengine ya kitaaluma," amesema.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Patrick Kitangula, amesema Serikali ilitoa muda wa kutosha wa watu wasiokuwa na sifa kujiendeleza takribani miaka minane na kusisitiza kuwa ambao hawana sifa wsitafute njia za mkato bali warudi shule.

Bodi hiyo pia imesisitiza kukuza maudhui ya ndani ambapo kupitia Mfuko wa Mafunzo ya Uandishi wa Habari watahakikisha upatikanaji wa mafunzo ya mara kwa mara kwa waandishi wa habari ili kuboresha utendaji wao na maendeleo ya sekta ya habari kwa ujumla.

Hatua hii ya bodi kuanza kusajili waandishi wa habari itasaidia kuimarisha weledi katika tasnia ya habari na kudhibiti usambazaji wa habari zisizo sahihi. 


Powered by Blogger.