MTENDAJI MKUU BRELA AELEZA MANUFAA USHIRIKIANO NA GS1
Na Nora Damian, The Page
MAKUBALIANO ya ushirikiano baina ya Taasisi inayosimamia msimbomilia nchini (GS1) na Wakala wa Usajili wa Majina ya Biashara na Leseni (BRELA) pamoja na taasisi nyingine za Serikali yameelezwa kuwa na manufaa makubwa katika kukuza biashara nchini.
Msimbomilia (Barcode) ni alama maalumu ya utambuzi inayotumika kutambua bidhaa halisi katika masoko mbalimbali duniani.
Leo Mei 20,2025 GS1 Tanzania imeingia makubaliano na taasisi tatu za Serikali ambazo ni BRELA, Shirika la Viwango nchini (TBS) na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma za biashara nchini.
Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, amesema ushirikiano baina yao na GS1 utaleta manufaa makubwa nchini na utachangia katika kuimarisha biashara na maendeleo ya viwanda.
“Tunajivunia kuwa na GS1 Tanzania kama mshirika wetu katika juhudi hizi muhimu na tunatarajia makubaliano haya yatazaa matunda mazuri kwa pande zote mbili, ni wakati wa kuunganisha nguvu zetu ili kuhakikisha kuwa tunalinda na kukuza miliki ubunifu na kuhamasisha vumbuzi, biashara na maendeleo ya uchumi katika nchi yetu.
“Kuna maeneo mengi ambayo ushirikiano wa karibu unaweza kuleta manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kukuza elimu ya biashara kwa wajasiriamali, kukuza tafiti katika eneo la miliki ubunifu, kupanua wigo wa soko la bidhaa zinazozalishwa nchini, kutoa usaidizi kwa wajasiriamali katika kuanzisha, kuendeleza, kukuza na kusimamia biashara zao kwa urahisi,” amesema Nyaisa.
Mtendaji huyo wa BRELA pia ameeleza majukumu muhimu ya wakala huo kama vile usajili wa makampuni, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, utoaji wa hataza, kutoa leseni za biashara na viwanda na kuhakikisha mifumo ya biashara inafanya kazi kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria.
“Huduma hizi ni muhimu kwa wajasiriamali, wabunifu na baishara kwa ujumla kwa sababu zinawalinda na kuwapa uhakika katika utekelezaji wa shughuli zao za kibiashara. Kwa kuzingatia majukumu haya ya msingi ushirikiano huu utaimarisha na kupanua ufanisi kwa pande zote mbili katika kuboresha mazingira ya biashara, kuhamasisha ubunifu na kuongeza ufanisi wa kiutawala wa kibiashara,” amesema.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amezipongeza taasisi hizo kutokana na kazi kubwa wanazofanya na kusisitiza ziendelee kuwa rafiki hasa kwa sekta binafsi ili kurahisisha shughuli za biashara nchini.
“Niipongeze taasisi yetu ya Brela mmeendelea kufanya kazi kubwa ya kusajili makampuni na majina ya biashara, na kazi hii inakwenda vizuri chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amejipambanua suala la uwekezaji, suala la biashara katika nchi yetu,” amesema Dkt. Jafo.
Waziri huyo pia ameziagiza taasisi hizo kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa nchini zina alama ya msimbolimilia ili ziweze kuuzwa katika masoko ya kitaifa na kimataifa hatua itakayowezesha pia kukabiliana na bidhaa bandia sokoni.
