WAZIRI MASAUNI AANZA ZIARA YA KIKAZI NORWAY
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni ameanza ziara ya siku tatu jijini Oslo, nchini Norway kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu wa masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Waziri Masauni amepokelewa Mei 11,2025 na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes.
Ziara hiyo imeratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Norway kufutia mwaliko uliotolewa kwa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Lengo la ziara hiyo ni kujifunza na kupata uzoefu kuhusiana na masuala ya mazingira, namna bora ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia biashara ya Kaboni na teknolojia ya kutenganisha taka katika miji na kuzifanya kuwa fursa na hatimaye kuzaliwa bidhaa na malighafi zingine ikiwemo mbolea, maji na nishati ya umeme.
Katika ziara hiyo Waziri Masauni atapata fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Norway akiwemo Waziri wa Hali ya Hewa na Mazingira wa Norway, Andreas Bjelland Eriksen, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Asmund Aukrust, Mkurugenzi Mkuu wa Norad, Bard Vegar Solhjell pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Maendeleo Endelevu katika Wizara ya Mambo ya nchi za Nje ya Norway.
Katika mikutano hiyo Waziri Masauni pamoja na viongozi hao watapata fursa ya kuzungumzia masuala mbalimbali ya mazingira pamoja na ushirikiano katika jitihada ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Aidha Waziri Masauni atapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Manispaa ya Oslo, Hafslunf Celsio pamoja na Kampuni ya Equinor.
Ujumbe wa Tanzania katika ziara hiyo umejumuisha Mwakilishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden, Mtaalaam kutoka kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) na wataalam kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
