WAZIRI MASAUNI AELEZA MKAKATI UTEKELEZAJI PROGRAMU MABADILIKO YA TABIANCHI
Na Mwandishi Maalumu, Copenhagen, Denmark
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Masauni ameeleta namna Tanzania inavyokabiliana na mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia njia mbalimbali vikiwamo vitu vya asili, kuweka mazingira rafiki kwa Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia hadi kufikia kiwango cha asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.
Mikakati mingine ni kuendelea kuzijengea uwezo taasisi zinazoratibu masuala ya biashara ya kaboni nchini.
Ameeleza hayo wakati wa mkutano wa kimkakati wa uwili (Bilateral Meeting) kati ya Tanzania na Viongozi wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ( Europian Union).
Mkutano wa majadiliano umefanyika Mei 7,2025 pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Mazingira Duniani unaoendelea jijini Copenhagen, Denmark.
Waziri Masauni amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Umoja wa Ulaya kuangalia namna bora ya kuiwezesha katika masuala ya kujengea uwezo, misaada ya kifedha yenye masharti nafuu, ruzuku na teknolojia ya upimaji wa kiwango cha kaboni.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wakuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya akiwemo Wopke Hoekstra, Kamishna wa Mazingira wa Ulaya, Krzysztof Bolesta ambaye ni Katibu wa Nchi Wizara ya Hali ya Hewa na Mazingira- Poland.
Bolesta amemwakilisha Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ambapo kwa sasa nchi ya Polend ndio Mwenyekiti wa EU.
Viongozi hao waliambatana na Christian Stenberg, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mazingira, Nishati na Fedha wa Denmark. Denmark inatarajiwa kuchukua uenyekiti wa EU ifikapo Julai mwaka huu.
Katika mkutano huo Waziri Masauni ameambatana na Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu masuala ya Mazingira na mabadiliko ya Tabianchi, Dkt. Richard Muyungi, Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden pamoja na wataalam kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Pamoja na masuala ya kubadilishana mawazo kuhusu vipaumbele kabla ya vikao vya Bonn na COP30, na Mwelekeo wa Nchi za kiafrika ambapo Tanzania ni mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika ( AGN).
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Sasa wa EU, Krzysztof Bolesta, ameipongeza Tanzania kwa hatua za kuanzisha Kituo cha Kaboni ambacho ni cha mfano kwa nchi za Afrika.
Aidha, alieleza kuwa siku zote Umoja wa Ulaya umekuwa ukifanya kazi na kuongoza kwa mfano mzuri na kwa kudumisha uwazi na haki na hivyo itaendelea kuhakikisha inatenda haki ya kutimiza ahadi zake zote za ufadhili wa programu za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchini.
Bolesta aliahidi kuendelea kushirkiana na Tanzania katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya Tabianchi.
