POLISI WATHIBITISHA KUMSHIKILIA GOLUGWA
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limesema linamshikilia Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara, Amani Golugwa kwa tuhuma za kusafiri nje ya nchi bila kufuata taratibu za kisheria.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na jeshi hilo leo na Kaimu Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Saalam imeeleza kuwa Golugwa amekamatwa Mei 13/2025 saa 06:45 usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere lango namba 3 akiwa katika maandalizi ya kusafiri kuelekea Brussels nchini Ubelgiji.
Katika taarifa hiyo Jeshi la Polisi limesema limemkamata Naibu Katibu Mkuu huyo kufuatia taarifa za siri kuwa amekuwa na mienendo ya kuondoka na kurudi nchini bila kufuata taratibu za kisheria.
Jeshi hilo hilo limesema linaendelea na uchunguzi wa kina wa taarifa hizo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama kuhusu suala hilo.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea na kupuuza taarifa za upotoshaji kuhusu hatua hizo za kisheria zinazomhusu Golugwa.
