WAZIRI MASAUNI AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KUTEMBELEA KAMPUNI YA UKUSANYAJI NA UCHAKATAJI TAKA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni ameongoza ujumbe wa Tanzania kutembelea Kampuni ya Hafslund Celsion inayojishughulisha na ukusanyaji na utenganishaji wa taka katika Manispaa ya Oslo nchini Norway.
Katika ziara hiyo Masauni aliambatana na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes, pamoja na maafisa kutoka Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.
Kupitia ziara hiyo ujumbe wa Tanzania ulipata fursa ya kujionea jinsi kampuni hiyo inavyotumia mbinu mbalimbali za ukusanyaji wa taka, jinsi invyotenganisha taka na kuzalisha bidhaa mbalimbali ukiwamo umeme.
Jiji la Oslo lina wakazi 725,000 ambapo kulingana na taarifa za mwaka 2023 kila mkazi huzalisha takribani kilo 157 za taka kwa mwaka. 
Kampuni ya Hafslund ilianza kazi ya utenganishaji taka mwaka 2012 na imekuwa ikitoa bure mifuko ya kuhifadhia taka ambapo mfuko wa kijani hutumika kwa taka za vyakula, mfuko wa tambarau taka za plastiki na taka nyingine huhifadhiwa katika mfuko mweupe.
Akielezea jinsi kampuni hiyo inavyofanya kazi Mshauri wa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo Mads Danielsen, amesema kampuni hiyo ina matawi matano ambayo yanajihusisha na upokeaji wa taka zitokanazo na mimea, vigae, vyuma chakavu, samani zilizovunjika na magodoro ambapo hujulikana kama taka zenye ujazo mwingi ( Bulky Waste).
Taka zingine ni zile hatarishi, taka zitokanazo na vifaa vya umeme na taka zinazoweza kurejelezwa kwa matumizi mengine.
Ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Jiji la Oslo wanatenganisha taka bila shurti, Danielsen amemweleza Waziri Masauni na ujumbe wake kuwa, wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kuelimisha umma ikiwa ni pamoja na sinema, redio, magazeti, vipeperushi, watu maarufu, mabango, matangazo kwenye vyombo vya usafiri, mitandao ya kijamii, mwongozo wa kutenganisha taka, maonesho na shughuli mbalimbali za uhamasihaji.
Utenganishaji huo wa taka umeiwezesha Kampuni ya Hafslund kuanzisha baadhi ya biashara kama uzalishaji maji yanayotokana na mvuke unaozalishwa baada ya kuunguza taka.
Biashara nyingine ni umeme, biashara ya Kaboni, uzalishaji wa nbolea na uuzaji wa vitu na vifaa vilivyotupwa ambavyo vinaweza kutumiwa na watu wengine.
Baada ya mkutano huo Ujumbe wa Tanzania ulipata fursa ya kutembelea kiwanda hicho na kujionea hatua mbalimbali za utenganishaji taka.
Kama nchi zingine duniani Tanzania nayo inazalisha taka hivyo, utenganishaji wa taka hutoa fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzalisha bidhaa zingine zenye manufaa na kuzalisha ajira.

