WATAHINIWA 134,390 KUANZA MTIHANI KIDATO CHA SITA
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limesema jumla ya watahiniwa 134,390 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha sita unaoanza kesho katika shule zote nchini.
Baraza hilo limesema pia watahiniwa 10,895 wanatarajiwa kufanya mitihani ya ualimu ngazi ya cheti na stahahada inayoanza kesho katika vyuo 68.
Akizungumza leo Mei 4,2025 na waandishi wa habari Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Said Mohammed, amesema maandalizi ya mitihani hiyo yamekamilika na kuwataka wasimamizi kusimamia kwa weledi na uadilifu ili kila mtahiniwa apate haki yake.
Aidha amewataka wakuu wa shule na wakuu wa vyuo kuzingatia mwongozo uliotolewa na baraza hilo na kuepuka kuingilia usimamizi ndani ya vyumba vya mitihani huku akionya kuwa hawatasita kukifuta kituo cha mitihani endapo watajiridhisha kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa mitihani.
