JESHI LA ZIMAMOTO LASISITIZA MATUMIZI SAHIHI NAMBA YA DHARURA 114
Na Nora Damian, The Page
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini limekemea vikali wananchi wanaotumia namba ya simu ya dharura kwa matumizi yasiyo sahihi na kuwataka waitumie pindi yanapotokea majanga ili liweze kuchukua hatua za kukabiliana nayo.
Onyo hilo limetolewa leo na Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini, Naibu Kamishna, Puyo Nzalayaimisi, wakati akizumgumzia maadhimisho ya Siku ya Wazimamoto Duniani inayoadhimishwa Mei 4 kila mwaka.
"Wananchi wengi sasa hivi wana uelewa wa namba ya dharura, sasa hivi hatuitiwi tu matukio ya moto, tunaitiwa matukio mengi ya uokoaji maana yake ni kwamba wananchi wameelewa.
"Wale ambao wamekuwa wakijaribu kutumia namba hii isivyo sahihi tunachukua hatua za kinidhamu ikiwemo kuwafikisha mpaka mahakamani," amesema Nzalayaimisi.
Aidha amesema jeshi hilo linaungana na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Wazimamoto Duniani akisema kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha wanalinda maisha na mali za Watanzania dhidi ya majanga mbalimbali.
"Hapa nchini tumeshuhudia matukio makubwa ya majanga ya moto, maporomoko lakini wazimamoto na waokoaji wetu waliweza kujitokeza kwa ujasiri kuokoa maisha na mali za wananchi," amesema.
Jeshi hilo limemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliwezesha katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi

