WANAFUNZI 100 SAMIA SCHOLARSHIP KUENDELEZWA FANI YA UTOAJI ELIMU KIDIGITALI
Na Nora Damian, The Page
Serikali imesema katika mwaka wa masomo wa 2025/2026 wahitimu 100 wa kidato cha sita watakaofanya vizuri zaidi na kuchaguliwa kujiunga elimu ya juu kupitia ufadhili wa masomo wa 'Samia Scholarship' watapelekwa nje ya nchi kujiendeleza katika taaluma ya utoaji elimu kwa njia ya kidijitali.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 7,2025 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, wakati akizungumza kwenye mkutano wa 18 wa kimataifa unaojadili matumizi ya Tehama na mifumo mbalimbali katika utoaji wa elimu (eLearning Africa).
Amesema lengo ni kuiwezesha nchi kuwa na wataalam katika taaluma hiyo hasa katika matumizi ya Akili Unde kwa kutumia lugha ya Kiswahili, utamaduni, mazingira na takwimu zetu ili kuwa na taarifa za kutosha.
"Hapa nchini tayari tunatumia eLearning na tuna mikakati ambayo tunaifanya kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania, tunashirikiana na Ngos mbalimbali kuhakikisha shule nyingi zaidi zinafikiwa na intaneti na kutumia vifaa mbalimbali kwa ajili ya kujifunza kama vile kompyuta.
"Kwenye bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha wanafunzi wanaofanya mtihani wa kidato cha sita sasa hivi watakaochaguliwa kupitia Samia Scholarship, wale watakaotaka kwenda kusoma nje tutawashindanisha ili kuzalisha wataalam wa taaluma hii," amesema Profesa Mkenda.
Mkutano unaofanyika kwa mara ya pili hapa nchini unashirikisha pia mawaziri wa elimu kutoka nchi 20 huku nyingine zikiwa zimetuma wawakilishi.
Unalenga kubadilishana mawazo na uzoefu kuhusu matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa elimu na kuendeleza ufahamu wa mifumo hiyo.
