'WAKULIMA TUMIENI TEKNOLOJIA YA MZURI PRO TIL' KUZALISHA KWA TIJA'
Na Nora Damian, The Page
Wakulima nchini wameshauriwa kuipokea teknolojia ya Mzuri pro til ili waweze kuzalisha kwa tija na ubora na kufikia malengo ya kuilisha dunia.
Teknolojia hiyo ina uwezo wa kufanya kazi zaidi ya moja shambani kama vile kulima, kulegeza udongo, kuweka mbolea na kupanda kwa wakati mmoja.
Akizungumza leo Machi 7,2025 Mkurugenzi wa Kampuni ya Mzuri Afrika yenye makao yake makuu Kurasini jijini Dar es Salaam, Shaaba Mgonja, amesema teknolojia hiyo imeingia nchini kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali yenye maono ya kulisha dunia.
Kampuni ya Mzuri Afrika inajihusisha na zana za kisasa za kilimo na ina kampuni pacha ya Agrami Afrika inayojihusisha na uagizaji, uuzaji na usambazaji wa mbolea za kimiminika zilizofanyiwa utafiti na kusajiliwa na mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa matumizi ya Tanzania.
"Teknolojia ya mashine ya Mzuri pro til zimetengezwa kwa ukubwa tofauti na zina uwezo wa kufanya kazi zote hizo.
"Mzuri pro til yenye ukubwa wa mita tatu ina uwezo wa kulima kulegeza udongo kuweka mbolea na kupanda heka saba na nusu kwa saa moja, nashine ya mita nne heka 10 kwa saa na mashine ya mita sita heka 15 kwa saa," amesema Mgonja.
Amesema teknolojia ya Mzuri Pro til imeingia nchini kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali yenye maono ya kulisha dunia na kwamba ujio wa teknolojia hiyo unakwenda kuleta uhalisia wa maana ya kulisha dunia.
"Ukiangalia wakulima wa mataifa yaliyotutangulia kwenye kilimo utaona ni jinsi gani wanawekeza kwenye teknolojia za kisasa za kilimo na matokeo yake huonekana wazi.
"Mfano mzuri ni uzalishaji wa ngano nchini Poland ukilinganisha na uzalishaji wa ngano hapa nyumbani ni vitu viwili tofauti," amesema.
Amesema Kampuni ya Mzuri Afrika inafanya kazi kwa karibu na kampuni ya Mzuri World ambapo rais wake amekuja kutembelea nchini kwa lengo la kuona ufanisi wa teknolojia hiyo.
Naye Rais wa Mzuri World, Mark Rozniak, amesema matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo zinaweza kuleta mabadiliko chanya kiuchumi kwa mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
"Teknolojia ya Mzuri pro til inazingatia utatuzi wa mabadiliko ya tabia nchi. Kwa kuliona hilo mashine hii inalima kilimo hifadhi ikijikita zaidi kwenye kutunza ardhi ya shamba kwa kulima theluthi mbili ya shamba na sehemu nyingine inapumzishwa kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo.
"Matumizi ya teknolojia ya Mzuri pro til inachochea utunzaji wa mazingira hivyo, nawahisi wakulima wa Tanzania kuipokea teknolojia hii ili kwa pamoja tukailishe dunia kwa kuzalisha kwa tija na ubora," amesema.
Kampuni hiyo tayari imeanzisha shamba darasa la ekari 300 na kituo cha mafunzo ya teknolojia ya mashine ya Mzuri pro til ili kutoa nafasi kwa Watanzania kujifunza kabla ya kusambaza teknolojia hiyo katika nchi nyingine barani Afrika.
Shamba darasa hilo litakuwa na mazao mchanganyiko katika mgawanyo sahihi ikiwemo sehemu ya kilimo cha mbogamboga na matunda, mazao jamii ya nafaka, mikunde, mazao jamii ya mizizi na mwngine ili kutoa fursa ya kujifunza kwa vitendo na kuchochea kilimo biashara kwa wakulima.
"Pamoja na shamba darasa pia tutakuwa na darasa la matumizi ya zana za kisasa za kilimo ikiwemo mashine ya Mzuri pro til ambapo Watanzania watapata nafasi kujifunza teknolojia hizo na hatimaye kujipatia ajira," amesema Mgonja.
