MFAHAMU HUSNA ANAYEFANYA KAZI MOCHWARI
Na Nora Damian, The Page
MIAKA ya nyuma haikuwa jambo la kawaida kukuta mwanamke akifanya kazi zilizoaminika kwamba ni za wanaume kama vile urubani, udereva, kuendesha mitambo mbalimbali, kuhudumia maiti na nyingine.
Kihistoria wanaume ndio waliaminika kufanya kazi hizo kwa miaka mingi lakini katika miaka ya karibuni hali imebadilika kwa wanawake kujitosa kuzifanya.
Husna Tangale (26) ni Mtaalamu wa Mochwari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke. Katika makala haya anaeleza kwanini alichagua kazi hiyo.
“Sikuwahi kufikiria kufanya kazi mochwari kwanza nilijua kwamba kazi hii inafanywa na wanaume, mimi nilipenda kuwa muuguzi kwahiyo baada ya kumaliza elimu ya sekondari nilisoma uuguzi. Lakini kuna mtu ambaye alinihamasisha mpaka kufikia hapa, aliniambia kwamba naweza nikasomea kozi ya mochwari ni kazi nzuri na wapo hadi wanawake.
“Kwahiyo nilikwenda kuongea na mume wangu akanishauri kama kweli nina nia na ninaweza kuifanya niende nikasome, nikaamua kwenda kusomea Mortuary Technician (Taaluma ya Mochwari) katika Chuo cha Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na baadaye nikafanikiwa kupata kazi hapa Temeke,” anasema Husna.
Hata hivyo anasema uamuzi wake ulipokelewa kwa mtazamo hasi na baadhi ya ndugu zake lakini alipiga moyo konde kwa kuwa anaichukulia kazi hiyo kama kazi nyingine ambazo watu wanakaa darasani na kufundishwa na haina uhusiano na dhana potofu.
“Kuna dhana potofu kuhusu watu wanaofanya kazi mochwari kama mimi, wengi wakisikia unafanya kazi hii wanakuwa na mitazamo tofauti, wanakuona si mtu wa kawaida, wanakuona kama mtu wa ajabu, wanakuona katili kwa sababu ilishazoeleka kwamba kazi hii kwa asilimia kubwa inafanywa na wanaume na watu wengine wanaihusisha na mambo ya ushirikina lakini kiukweli tumesomea kazi hii.
“Mimi nilivyoamua kuifanya baadhi ya ndugu zangu walinishangaa, mama aliniuliza…‘wee mtoto ujasiri huo umeupata wapi’ lakini kwa sasa wameanza kunielewa, namshukuru sana mume wangu aliniunga mkono,” anasema Husna ambaye ni mama wa mtoto mmoja.
KAZI ZAKE ZA KILA SIKU
Husna anasema kazi zake ni kuhakikisha kuwa mwili umepokewa kwa utaratibu na kuhifadhiwa kisha huandaliwa kwa ajili ya taratibu za maziko.
Anasema hata kama ni mwili uliopata ajali hutengenezwa na kurudishwa viungo mahali pake na kuwa na mwonekano mzuri kazi ambayo huifanya kwa kushirikiana na wenzake.
“Tunashughulika kupokea miili, kuiandaa na kuiweka kwenye mwonekano mzuri. Hata kama ni mwili wa ajali umekatika mikono au miguu inabidi utengeneze uwe na mwonekano mzuri ili ndugu wanapokuja wautambue.
“Sipati ugumu wowote kwa sababu naipenda kazi yangu, sioti ndoto za ajabu na wala sijawahi kuona vitu vya ajabu...hata nikiingia zamu usiku nakuwa peke yangu sipati hofu,” anasema Husna.
CHANGAMOTO
Changamoto katika kazi yake ni pale ndugu wanapofika kutambua au kuchukua miili ya wapendwa wao wanapokuwa wanalia lakini anasema wamefundishwa kuwatuliza wafiwa kwa kuwajenga kisaikolojia ili warudi katika hali zao za kawaida.
“Tunakutana na changamoto mbalimbali pale ambapo ndugu wanakuja wanalia, sasa na mimi nikilia je, ninayemhudumia itakuwaje…lakini tumepata mafunzo na tuna uzoefu. Mojawapo ya huduma unatakiwa ukae chini uongee naye, umfariji anapokaa sawa unaanza kumhudumia…unaweza kumpigisha stori mpaka akacheka, tunamuonyesha upendo, watu wa mochwari tuna upendo na si kama tunavyodhaniwa mtaani,” anasema Husna.
WENZAKE WANAVYOMZUNGUMZIA
Mohamed Ally ni Mkuu katika Chumba cha Kuhifadhia Maiti Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, anasema Husna ametukuka katika utendaji wake wa kazi na ana weledi mkubwa.
“Ni mtaalamu aliyebobea katika kuhudumia miili, yuko vizuri taratibu zote anazifahamu, ni binti wa mfano, ametulia, ana nidhamu kwa wakubwa zake na hata walio chini yake.
"Hapa mochwari tunao mabinti wawili, tunaishukuru Serikali imefanya jambo zuri kwa kuzingatia jinsia kwa maana ya kuwa na wafanyakazi wanawake na wanaume katika mochwari,” anasema Ally.
USHAURI KWA WANAWAKE
Husna anawashauri wanawake kutochagua kazi anasema; “Unaweza kusomea uuguzi au taaluma ya dawa lakini ni vizuri pia kuangalia kitu gani ambacho kina uhitaji. Kama kijana, dada au mama hutakiwi kuchagua kazi, kazi yoyote ambayo ni halali ifanye.
“Mwingine ukimwambia unafanya kazi mochwari anashtuka na kukushangaa, anakuambia umewezaje, kikubwa katika karne hii wanawake tufanye kazi kwa bidii lakini tusifanye kazi haramu, tufanye kazi ambazo ni halali kwa mujibu wa sheria,” anasema Husna.
Husna anasema tayari amemuhamasisha wifi yake kuingia katika fani hiyo ambaye kwa sasa anafanya kazi mochwari katika hospitali moja jijini Dar es Salaam.
“Najivunia kuwa hapa Temeke, nina furaha na naipenda kazi yangu, nakutana na watu mbalimbali, tunatengeneza undugu, mtu anapotoka hapa unamkabidhi mwili anakwenda mkoani akifika anakupigia simu kukushukuru na siku nyingine ikitokea tatizo anakutafuta,” anasema Husna.
Husna Tangale (Kulia) akiwa na mwandishi wa makala haya.
