DKT. SCHOLASTIKA KEVELA: TUGOMBEE UONGOZI TUWATETEE WANAWAKE

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) katika Mkoa wa Njombe, Dkt. Scholastika Kevela, akiwa katika shughuli za chama.


Na Nora Damian, The Page

MOJA ya maazimio ya Mkutano wa Beijing uliofanyika mwaka 1995 nchini China ni kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa za kushiriki katika uongozi na utawala.

Mwaka huu ikiwa imetimia miaka 30 tangu kufanyika kwa mkutano huo, Siku ya Wanawake Duniani inayosherehekewa Machi 8 kila mwaka inatumika kufanya tathmini ya utekelezaji wa maazimio ya Beijing ikiwemo suala la kuongeza ushiriki sawa wa wanawake katika uongozi.

Tanzania kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha inatekeleza maazimio ya Beijing hasa katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi.

Katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake mwaka huu Kaulimbiu ‘Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji’ inajielekeza kuhamasisha jamii kukuza usawa, haki na uwezeshaji wanawake na wasichana kwa kuzingatia kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 ili wajiamini na kujiandaa na kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Dkt. Scholastika Kevela ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) katika Mkoa wa Njombe, ambaye anasema uongozi haujatengwa kwa ajili ya watu fulani bali ni kwa ajili ya watu wote hivyo wanawake wasijione wanyonge wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.“Wakati ukifika tuchukue fomu tugombee ili tuweze kushika uongozi tuwatetee wanawake wenzetu ambao bado hawajapata fursa ya kuwa viongozi. Akijitokeza mwenzetu anagombea tusimkatishe tamaa, tumpigie kura, tumtie moyo kwa sababu kadiri tunavyokuwa na viongozi wengi wanawake maendeleo ya haraka yanapatikana,” anasema Dkt. Kevela.

Anasema mwanamke si kiumbe dhaifu katika kufikiri na wala kufanya kazi na hata akili alizonazo mwanamume ndio alizonazo mwanamke.

“Mwenyezi Mungu wakati anamuumba mwanadamu si kwamba aliongeza akili nyingi kwa mwanamume, kwamba awe na akili nyingi halafu mwanamke awe na akili ndogo, hapana ni tofauti tu ya maumbile lakini akili alizonazo mwanamume ndio alizonazo mwanamke.

“Kulikuwa na mfumo dume ambao uliwakandamiza wanawake, walikuwa hawana ruhusa ya kuchagua wala kuchaguliwa, kazi yao ilikuwa kupika, kufua yaani mama wa nyumbani lakini tunashukuru hivi sasa tunaona wanawake duniani wameshika hatamu katika nafasi za uongozi. Wengine ni marais, wabunge, mawaziri na nchini kwetu ‘role model’ wetu ni Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Ameishangaza dunia si kwamba ni bahati mbaya, kichwani anao uwezo, tunamuona anafanya kazi nyingi ndiyo maana wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa na mimi nikiwemo tumempitisha kwa asilimia 100 apeperushe bendera kwa sababu amefanya kazi nzuri miradi ya maendeleo inatekelezwa karibu maeneo yote ya nchi, ameimarisha utawala bora na amedumisha amani…ni shujaa wetu Watanzania, ni shujaa wa dunia, kaipeleka Tanzania duniani nchi yetu inaonekan.

“Kwa wanawake tuone kwamba viongozi wakubwa ni ‘role model’ wetu hivyo, sisi tufanye kazi kwa bidii, tujae kwa nafasi zetu, nyakati za kusema kwamba ukae utawezeshwa hazipo… wanawake wenzangu wa Mkoa wa Njombe tunyanyuke tufanye kazi kwa bidii,” anasema Dkt. Kevela.

Anasema pia Mkoa wa Njombe unang’ara kiuchumi, kisiasa na kijamii na akiwa kiongozi wa kinamama amekuwa akitumia nafasi hiyo kuwahamasisha wanawake kugombea uongozi na kutolea mfano hata katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba mwaka jana wengi walichomoza katika uongozi wa vijiji.

“Nimekuwa nikizunguka kusaidia wahitaji, nimeanzisha miradi ya viwanda vya kutengeneza sabuni, nimewahamasisha kinamama kugombea ndio maana wenyeviti wa vijiji kule Njombe wako wengi wanawake, nawaomba kinamama wenzangu wa Mkoa wa Njombe wakati ukifika ni haki ya kila mtu anayetaka kuwa diwani au mbunge isipokuwa fomu ya rais tumeshamaliza,” anasema.

Dkt. Kevela anawashauri wanawake kuendelea kuzingatia majukumu yao ya msingi ya ulezi katika familia ili kupunguza au kumaliza kabisa vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa vikitokea katika maeneo mengi kila uchao.

“Pamoja na kwamba tunatafuta nafasi za uongozi ile nafasi ambayo alitukabidhi mwenyezi Mungu ya kuzaa kwa uchungu tuangalie wale viumbe tunaozaa kwa uchungu, tuwalee kwa umakini. Watoto wetu wanafanyiwa vitu vya ajabu ni sisi wanawake wa kutulia chini na kuweza kulea vizuri watoto wetu,” anasema.

TUZO YA SAMIA

Dk. Kevela anasema Tuzo Maalumu ya Kimataifa ya The Gates Goalkeeper Award aliyotunukiwa Rais Dkt. Samia na Taasisi ya Gates ya Marekani, ni halali yake.

Tuzo hiyo aliyokabidhiwa hivi karibuni hutolewa kwa viongozi waliowezesha nchi zao kuharakisha maendeleo kuelekea kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Rais Samia ni kiongozi wa kwanza barani Afrika kupokea tuzo hiyo akitunukiwa katika kipengele cha mapambano dhidi ya vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga chini ya miaka mitano.

“Rais Samia anastahili na amepata tuzo ile si kwa upendeleo, ni haki yake kwa sababu amepunguza vifo vingi vya wanawake na watoto, tunampongeza sana ni ‘role model; wa wananchi wa Tanzania,” anasema Dkt. Kevela.

Taasisi ya Gates wameangalia zaidi jitihada anazozifanya Rais Samia katika mapambano ya afya ya uzazi ambayo yamewezesha kubadili namba za Tanzania katika historia ya dunia kwa habari ya vifo vya akina mama na watoto chini ya miaka mitano.

Dkt. Kevela anasema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kielelezo cha mafanikio ambayo mwanamke anaweza kuyafikia na kuwataka wanawake waige mfano huo kwa kujitokeza kwa wingi kugombea katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.



Powered by Blogger.