MHANDISI MRAMBA: HAKUNA UPUNGUFU WA UMEME, TUNAIMARISHA UPATIKANAJI MIKOA YA KASKAZINI
Na Nora Damian, The Page
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema uamuzi wa Tanzania kununua umeme kutoka nchini Ethiopia haumaanishi kuwa nchi iko katika changamoto ya upungufu wa umeme bali inalenga kuimarisha upatikanaji katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Akizungumza leo Machi 10,2025 Mhandisi Mramba amesema Mikoa ya Kanda ya Kaskazini kwa sasa inatumia umeme unaozalishwa katika Mikoa ya Kusini.
Amesema umeme utakaonunuliwa kutoka nchini Ethiopia utapitia Kenya hadi Namanga mkoani Arusha na hatua hiyo ina faida kwa pande zote mbili kwa kuwa njia itakayotumiwa kununua umeme nchini Ethiopia ndio hiyo itakayotumiwa kuuza umeme kwa nchi zenye uhitaji.
"Sehemu ya mikakati ya kuimarisha umeme nchini ni pamoja na kununua umeme kutoka nje na ni sehemu ya sera ya taifa ya nishati, na kuuziana umeme ni sehemu ya mipango ya kuimarisha umeme kwa nchi zote si kwa Tanzania tu. Ndiyo maana Serikali inaingia gharama kujenga njia za usambazaji umeme," amesema Mhandisi Mramba.
Kwa mujibu wa Mramba, mpaka sasa Tanzania inazalisha umeme wa kutosha megawati 3,796 na wanaendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tanzania kwenda Zambia ambapo itakapokamilika itatoa fursa kwa Tanzania kuuza umeme kwa nchi za Kusini mwa Afrika.
Hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kununua nishati ya umeme kutoka nje ya nchi, kwa sasa umeme wa Mkoa wa Kagera unatoka nchini Uganda kwa kuwa mkoa huo hauko kwenye Gridi ya Taifa.
Vilevile Mkoa wa Rukwa unatoa nishati yake ya umeme kutoka mji wa Mbala ulioko nchi ya jirani ya Zambia.
