KILWA YAENDELEA KUFURIKA WATALII
Na Beatus Maganja
Meli ya Kifahari ya kitalii ya 'Le Bougainville' imewasili katika Hifadhi ya urithi wa utamaduni wa dunia Magofu ya Kale Kilwa Kisiwani na Songo Mnara mkoani Lindi.
Meli hiyo imewasili leo Machi 5,2025 ikiwa na watalii 133 kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa shughuli za utalii ikiwa ni safari yake ya saba tangu kuanza kwa msimu wa utalii wa mwaka 2025.
Watalii waliotembelea hifadhi hiyo wametoka Mataifa ya Denmark, Australia, Canada, Ufaransa, Marekani, Uingereza na Afrika Kusini huku wengine wakitokea Mataifa ya Uswisi, Romania, Ujerumani, Ubelgiji, New Zealand na Ireland.
Meli hiyo ya kifahari inahudumia wageni kutoka pande zote za dunia, ikitoa fursa kwa watalii kutembelea maeneo ya kihistoria na kiutamaduni ya Kilwa ambayo ni urithi wa dunia wa UNESCO na kuwawezesha watalii kushuhudia tamaduni za asili zinazopatikana katika hifadhi hiyo ya kipekee iliyo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Kwa mujibu wa maofisa wa hifadhi hiyo, safari hiyo ni sehemu ya juhudi za kuendeleza utalii wa kipekee katika mikoa ya Kusini huku wakisisitiza umuhimu wa utalii endelevu ambao unaleta faida kwa jamii za maeneo husika.
Hiyo ni meli ya saba kuwasili katika hifadhi hiyo tangu kuanza kwa mwaka huu ambayo mpaka kufikia leo imefikisha jumla ya watalii 854 na inatarajiwa kuongeza idadi ya wageni zaidi katika miezi ijayo.
Wageni wamepata fursa ya kujifunza mengi kuhusu historia ya Kilwa, ikiwa ni pamoja na magofu ya Kilwa Kisiwani maeneo ambayo yalikuwa ya kibiashara na utawala katika zama za utawala wa Kiarabu na Ureno, pia wamepata fursa ya kushirikiana na jamii za wenyeji.
Meneja wa Hifadhi ya Kilwa, Mhifadhi Mwandamizi (Malikale) SC Kelvin Stanislaus Fella amesema; "Tuna furaha kuona meli ya 'Le Bougainville' ikirudi tena na na kuleta wageni kutoka mataifa mbalimbali. Hii ni fursa kubwa kwa utalii wetu na ni hatua muhimu katika kutangaza Kilwa kama kivutio cha kimataifa."
Meli ya 'Le Bougainville' ni miongoni mwa meli za kifahari zinazotumia njia za baharini kutoa huduma za utalii katika maeneo ya Afrika Mashariki huku safari hizo zikiratibiwa na Kampuni ya Akorn ambayo huwapeleka watalii katika maeneo mbalimbali duniani na inatarajiwa kuleta wageni wengi zaidi katika msimu wa utalii wa 2025.


