DABI YA MACHI 8: POLISI YAONYA MASHABIKI KWENDA NA MATOKEO
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema wamejipanga vyema kuelekea mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga uliopangwa kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa wikiendi hii na kuwatahadharisha mashabiki wasiende uwanjani wakiwa na matokeo mfukoni.
Kamanda Muliro amesema leo Machi 5,2025 kuwa kutokana na uzito wa mchezo huo na kiwango cha mashabiki wanaotarajiwa kuingia uwanjani watahakikisha watu wanakwenda kwenye burudani na si kwenda kufanya vitendo vya kijinai.
Aidha amewataka mashabiki kukata tiketi mapema na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litakapotangaza muda wa kufungua mageti waingie uwanjani mapema kuepuka msongamano ambao unaweza kusababisha kutendeka kwa vitendo vya kijinai.
"Jeshi halitavumilia vitendo vya kijinai vitakavyojitokeza kwenye uwanja ambavyo ni kinyume na taratibu, desturi na mila la Watanzania.
"Jeshi la Polisi litakuwa tayari kutimiza majukumu yake bila woga au kumwonea mtu yeyote na tunaendelea kusisitiza wanasoka wasiende uwanjani na matokeo yao mfukoni," amesema Kamanda Muliro.
