BRELA YAFUTA KAMPUNI 11 ZINAZOENDESHA BIASHARA YA UPATU
Na Nora Damian, The Page
Kampuni 11 zilizobainika kuendesha biashara ya upatu zimefutwa rasmi na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Uamuzi huo wa BRELA umekuja siku chache baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuwakamata watu 26 wakiwemo viongozi wa Kampuni ya LBL kwa tuhuma za kuendesha biashara ya upatu.
Kampuni hizo zimekuwa zikiwahamasisha wananchi kujiunga kwa kulipa Sh 50,000 na kuendelea kwa ahadi ya kupata faida kubwa kwa muda mfupi.
Akitangaza uamuzi huo leo Machi 5,2025 Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, amesema kampuni za LBL zilisajiliwa kati ya Novemba 2024 na Januari 2025 na zimefutwa rasmi tangu Februari 27,2025.
"Sababu za kufuta kampuni hizo ni kukiuka masharti ya Kifungu cha 400A (1) (e) cha Sheria ya Kampuni kwa kufanya shughuli za kibiashara nje ya madhumuni yaliyoainishwa katika Katiba za kampuni hizo na miongozo ya uendeshaji wa kampuni wakati wa usajili.
"Kifungu hiki kikikiukwa sheria inamtaka Msajili kuchukua hatua chini ya Kifungu hicho 400A (1) (e) ambazo ni kuijulisha kampuni kuhusu ukiukwaji na hatua anazokusudia kuzichukua kwa kampuni husika. Sheria inaendelea kueleza kuwa, endapo kampuni itashindwa kutoa maelezo, au kutoa maelezo yasiyoridhisha, Msajili atafuta kampuni husika kwenye Rejista ya Kampuni," amesema Nyaisa.
Kulingana na BRELA, kampuni husika zilipewa notisi ya kusudio la kufutwa kati ya Januari 2 na 26,2025 lakini hazikuwasilisha maelezo yoyote kama zilivyotakiwa chini ya kifungu 400A (2).
Kampuni zilizofutwa ni LBL Mtwara Media Company Limited, LBL Morogoro Media Company Limited, LBL Geita Advertising Media Limited, LBL Mbeya Media Limited na LBL Future Vision Advertising Agency Company Limited.
Nyingine ni LBL Mbezi Advertising Media Company Limited, LBL Ubungo Media Limited, LBL Mabibo Media Company Limited, LBL Mbagala Media Company Limited, LBL Gongo la Mboto Media Advertising Company Limited na LBL Dar es Salaam Kigamboni Advertising Company Limited.
Mtendaji huyo wa BRELA amesema biashara ya upatu ni kinyume na sheria za nchi na amewahimiza wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika zikiwemo taasisi za Serikali na Jeshi la Polisi ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya kampuni au watu wanaofanya au kujihusisha na biashara hiyo.
