PforR YALETA UTULIVU KWA JAMII YA MVUMI
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mratibu wa Programu ya Lipa kwa Matokeo (PforR), Wizara ya Maji Mhandisi Mashaka Sita pamoja na timu ya Benki ya Dunia wamekagua hali ya huduma ya maji katika Wilaya ya Chamwino, ambapo ukaguzi umefanyika katika huduma ya majisafi Chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii Mvumi Mission.
Imeonekana chombo hicho cha watumia maji kujidhatiti kwa kupiga hatua kuanzia kutoa huduma na kupanga kuongeza mtandao wa maji ili kuwafikia wananchi wengi, ambapo huduma ya maji inapatikana kwa saa 12.
“Kujaza maji ndoo moja inatakiwa iwe chini ya dakika tano, na isizidi," Mhandisi Sita amesema na kuainisha kuwa hiyo ni moja ya kigezo cha kupima ubora wa huduma ya maji yenye kiwango katika jamii.
Diwani wa Kata ya Mvumi, Keneth Chiute, pamoja na kushukuru kwa mradi kwa kuondoa adha iliyokuwepo, ameomba nguvu zaidi itumike kuwafikia baadhi ya wananchi katika maeneo mengine ambao wanatamani mradi kuwafikia.
Naye Diwani wa Viti Maalumu, Shukran Chelea, ameainisha kuwa PforR imeleta utulivu katika ndoa katika jamii yao kwa sababu huduma ya maji ilikuwa inatafutwa usiku, isiyokuwa na uhakika, hivyo kwa mradi wa maji uliofanikishwa na programu ya PforR hivi sasa familia na mahitaji mengine ni imara zaidi.
Vyanzo vya huduma ya maji katika Wilaya ya Chamwino ni chini ya ardhi, hivyo utunzaji wa mazingira ni jambo muhimu ili kuwa na huduma endelevu ya maji katika jamii.
Kazi hiyo ya ukaguzi wa utekelezaji wa PforR imeongozwa na Toyoko Kodama wa Benki ya Dunia kutoka Marekani.
Tanzania imefanya vizuri katika programu hiyo na kuwa darasa kwa nchi nyingine duniani kujifunza ili kufikisha huduma za maji za uhakika kwa wananchi.
