HAKUNA ATAKAYEKOSA ARVs - SERIKALI
Na Nora Damian, The Page
Serikali imewatoa hofu Watanzania na kuwahakikishia kuwa imejiandaa vya kutosha kuhakikisha Dawa za Kupunguza Makali ya Virusi vya Ukimwi (ARVs) zinapatikana wakati wote na kila anayehitaji anapata.
Hivi karibuni Rais wa Marekani, Donald Trump, alitangaza kusitishwa kwa misaada ya ARVs kwa nchi mbalimbali za Afrika hatua iliyozua hofu miongoni mwa nchi zilizokuwa zikipokea misaada hiyo.
Akizungumza leo Machi Mosi,2025 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali haitaishiwa dawa na hakuna mtu atakayekosa dawa.
“Watanzania wasiwe na hofu, Serikali ina afua nyingi za kuwahudumia, inashirikiana na wadau wa maendeleo. Kama nchi tumejiandaa, kama fedha zitasitishwa, tumetenga fedha tutanunua ARVs Watanzania wenzetu waendelee kuishi …hatutaishiwa na hatutakosa dawa,” amesema Msigwa.
Msemaji huyo wa Serikali pia amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari ya kujilinda dhidi ya ugonjwa huo kwa kuwa Ukimwi bado upo.
“Tuendelee kuchukua tahadhari Ukimwi bado upo, tujikinge ili tuumalize, Watanzania tuwe wa kwanza kuumaliza na inawezekana,” amesema Msigwa.
