SH TRILIONI 1.2 ZAIMARISHA HUDUMA ZA AFYA, VIFAA TIBA

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, akizungumza na waandishi wa habari kuelekea miaka minne ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Na Nora Damian, The Page

Serikali imewekeza zaidi ya Sh trilioni 1.2 katika eneo la huduma za afya ya msingi na vifaa tiba kwa kipindi cha miaka minne ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Uwekezaji huo umewezesha kujengwa kwa hospitali za wilaya 129, kukarabati hospitali kongwe 48, kujenga vituo vya afya 367, kukamilisha zahanati 980 zilizoanza kujengwa na wananchi, kujenga nyumba 270 za watumishi, majengo ya dharura 86, ICU 30, kujenga mitambo 21 ya hewa ya oksijeni. 

Hayo yamesemwa leo Machi Mosi,2025 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo itatimia Machi 19,2025.

“Hatujisemei sisi Tanzania, vyombo vikubwa vya kimataifa vimeona juhudi kubwa za Rais Samia katika kuimarisha sekta ya afya, na hivi karibuni alitunukiwa tuzo ya kimataifa (The Great Goalkeeper) na Taasisi ya Gates...kazi iliyofanyika ni kubwa,” amesema Msigwa.

Kulingana na Msigwa katika kipindi cha miaka minne zahanati 677, vituo 425, hospitali 100 vimepatiwa vifaa tiba na vituo 129 vimefungwa hewa tiba ya oksijeni.

Aidha amesema katika kipindi hicho yamenunuliwa magari ya kubebea wagonjwa 382, magari 210 ambayo yamesambazwa kwa waratibu wa mikoa na pikipiki 540 kwa ajili ya huduma za Mkoba.

“Katika kipindi cha miaka minne Serikali imeajiri watumishi 25,936, imeongeza bajeti ya vifaa tiba kutoka Sh bilioni 35 hadi Sh bilioni 181, X – Ray zimeongezeka kutoka 114 hadi 431, Ultrasound kutoka 384 hadi 792 na bajeti ya dawa imefikia Sh bilioni 239. Wataalam wabobezi wameongezeka kutoka 69 hadi 338,” amesema.

VIONGOZI WA MIKOA, WILAYA

Msigwa amesisitiza kwa viongozi wa mikoa na halmashauri za wilaya kutumia redio za kijamii zilizoko katika maeneo yao kutoa taarifa namna ambavyo serikali imetekeleza majukumu yake.

Amesema ni haki ya wananchi kujua yale yaliyofanywa na Serikali na tayari taasisi mbalimbali za Serikali zimeanza kueleza kwa umma yaliyofanywa na Serikali kwa kipindi cha miaka minne zoezi linaloratibiwa na Idara ya Habai – Maelezo ambalo lilianza Februari 16 na linatarajiwa kuhitimishwa Machi 27,2025.

“Tarehe 27 ikifika nitakusanya taarifa zote na nitampelekea Waziri Mkuu waliotoa taarifa, hatutaki mtu mwingine apotoshe wakati sisi tupo,” amesema Msigwa.

Kwa mujibu wa Msigwa, kuanzia Aprili 14,2025 mawaziri wataanza kutoa taarifa kuhusu yale yaliyotekelezwa na Rais Samia kutokana na ahadi alizoziweka.


Powered by Blogger.