WATANZANIA WASIOGOPE SARATANI INATIBIKA
Wakati takwimu zikionyesha Watanzania 55,000 wanapata saratani kila mwaka, wito umetolewa kwa jamii kutoogopa kwa kuwa ugonjwa huo unatibika.
Stella Meshack na Ramadhani Mussa ambao wameugua saratani ya titi ni kati ya Watanzania wengi ambao wamepata matibabu na kupona.
Meshack na Mussa wametoa shuhuda hizo Februari 4,2025 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani yenye Kaulimbiu 'Ungana kwa upekee'.
"Nilianza kuugua mwaka 2019 nilipata uvimbe kwenye titi na baada ya uchunguzi niligundulika kiwa na saratani ya titi. Niliogopa lakini nilipata ushauri na kuanza matibabu.
"Watu wengi wamekuwa wakiogopa matibabu na kuishia njiani lakini mimi nawashauri wasiache matibabu kwa sababu kansa inatibika...mimi nimetibiwa na mpaka leo naendelea kuishi," amesema Stella.
Naye Ramadhani Mussa aliyepata saratani ya titi amesema alianza kuona dalili mwaka 2005 na kuanza matibabu katika Hospitali za Mwananyamala, Muhimbili hadi Ocean Road na kwa sasa anaendelea vizuri.
"Dalili nilianza kuziona tangu mwaka 2005 yalianza kutoka majimaji katika titi langu la kushoto, nilifanyiwa vipimo na kuambiwa ni ugonjwa wa kawaida unatibika.
"Mwaka jana (2024) nilianza matibabu Ocean Road, nawashukuru sana kwa sababu nilizeeka kabisa kwa sababu ya saratani lakini sasa hivi naonekana kijana na maisha yanaendelea.
"Watanzania wasiogope, saratani inatibika kwahiyo wafike hospitali kupata matibabu, kansa ya titi wanaume pia inatuhusu," amesema Mussa.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Waziri wa Afya, Jenister Mhagama ambaye aliwakilishwa na Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Afya ya Mama na Mtoto, Dk. Mzee Nassor, amesema Serikali imeongeza wigo wa upatikanaji huduma za kuzuia na kudhibiti saratani.Amesema Serikali imeongeza vifaa tiba vya kisasa vya uchunguzi, kupatikana kwa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi kwa gharama nafuu.
Aidha amewataka wazazi kuwakinga watoto wa kike dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi kwa kuwapeleka kupata chanjo ya HPV kwa kuwa ni salama na imethibitishwa na Serikali.
"Awali chanjo ya HPV ilikuwa inatolewa mara mbili lakini siku hizi ni mara moja tu, kwahiyo wasichana wengi wanapatiwa ili iwazuie na saratani ya mlango wa kizazi na tunatarajia baadaye tatizo hili litapungua.
"Chanjo zimethibitishwa kuwa ni salama kwahiyo nawahimiza wazazi wawaruhusu watoto wao wa kike wapate chanjo ili kuzuia saratani ya mlango wa kizazi katika maisha yao yajayo," amesema Dk. Nassor.
Mkurugenzi huyo amesema Serikali imechukua hatua kukabili magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanashika kasi na kusisitiza wananchi kuzingatia ulaji unaofaa ikiwemo kula mbogamboga na matunda, kupunguza vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi na sukari nyingi.
"Tuache tabia bwete, tufanye mazoezi kwa kuushughulisha mwili angalau dakika 30 mara tano kwa wiki," amesema Dk. Nassor.
Pia amezielekeza halmashauri kutenga bajeti kuhakikisha huduma za saratani zinapatikana hadi katika ngazi ya zahanati ili kuongeza wigo wa kugundua mapema na kuchukua hatua.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Ocean Road, Dk. Diwani Msemo, amesema kwa mwaka wanapokea wagonjwa wapya 7,500 huku ikikadiriwa kwamba watu 55,000 wanapata saratani kila mwaka hapa nchini.
Dk. Msemo amehimiza jamii kujenga umoja na mshikamano na kuepuka unyanyapaa kwa watu wanaougua saratani.
