FCC YATUNUKIWA ITHIBATI YA UBORA KIMATAIFA

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), William Erio, akizungumza wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) William Erio, amesema Watanzania na mataifa mbalimbali yategemee huduma bora zaidi kutokana na tume hiyo kupata Cheti cha Ithibati cha Utoaji wa Huduma bora kwa Viwango vya Kimataifa (ISO).

Ameyasema hayo leo Februari 6,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na kusema watazingatia ubora wa huduma wanazotoa kwa wananchi ili kuendana na ithibati waliyopata.

Aidha amesema Sheria ya Ushindani iliyofanyiwa marekebisho hivi karibuni itarahisisha ufanyaji biashara na uwekezaji na kulishukuru Bunge na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipitisha.“Kwa sasa mchakato wa marekebisho umeanza kwa Sheria ya Alama za Bidhaa ili kuhakikisha inarekebishwa na kuakisi hali ya sasa ya maendeleo ya biashara duniani,” amesema Erio.

Kuhusu kikao hicho amesema kinalenga kuvijengea uwezo vyombo vya habari kuhusu shughuli zinazofanywa na tume hiyo ili viweze kuufikishia umma taarifa sahihi.

Katika kikao hicho mada mbalimbali zilitolewa ambazo ni kuhusu maboresho ya sheria, mienendo ya kibiashara inayokatazwa na sheria ya ushindani, tafiti, miungano ya makampuni na uraghbishi pamoja na udhibiti wa bidhaa bandia nchini.

Tume hiyo ina majukumu makubwa mawili ya kushajihisha ushindani ili kuhakikisha kunakuwepo na ushindani sahihi kwa biashara pamoja na kumlinda mlaji.


Powered by Blogger.