DC BARIADI AKEMEA VITENDO VYA KUCHUNGA MIFUGO NDANI YA HIFADHI
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga amekemea vitendo vya baadhi ya wafugaji wilayani humo kuchungia mifugo ndani ya hifadhi hususani Pori la Akiba Maswa.
Amesema wilaya hiyo si sehemu salama kwa watu wanaofanya ujangili na wanaovunja sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 6, 2025 wilayani humo Simalenga amesema vitendo hivyo vimekuwa vikileta athari kubwa kwa mazingira ya hifadhi na kuhatarisha usalama wa wafugaji wanaoingia ndani ya hifadhi dhidi ya wanyamapori wakali pamoja na kuharibu mfumo ikolojia wa maeneo hayo.
"Niwasihi wananchi wote walio ndani ya Wilaya ya Bariadi, maeneo ya Pori la Akiba Maswa, maeneo ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kipande kinachoingia wilaya ya Bariadi Kata ya Matongo si maeneo ya kwenda kuchunga mifugo wala haifai kwenda kuingiza mifugo," amesema Simalenga.
Katika hatua nyingine Ofisa Habari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA, Beatus Maganja, akiongea na wananchi wa Kijiji cha Halawa wilayani humo wakati wa programu ya utoaji elimu, amebainisha athari mbalimbali zinazoweza kusababishwa na vitendo vya kuchungia mifugo ndani ya hifadhi.
Amezitaja athari hizo kuwa ni pamoja na ushindani wa malisho unaotokana na mwingiliano kati ya wanyamapori na wanyama wafugwao ambao unaweza kusababisha wanyamapori kupoteza maeneo yao ya asili ya kulisha au maji.
Maganja amesema wanyamapori wanapohisi tishio la upungufu wa malisho yao ya asili wakati mwingine huhama na kuelekea maeneo mengine ikiwemo makazi ya watu na hivyo kupelekea migongano kati ya binadamu na wanyamapori.
Naye CI Lusato Masinde Ofisa Uelimishaji kutoka Kanda ya ziwa ya TAWA, amesema katika kuhakikisha usalama wa wananchi wa vijiji 32 vinavyozunguka hifadhi hiyo TAWA kupitia Pori la Akiba Maswa wamekuwa wakitoa elimu ya mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi hao.
Amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2024 mpaka Januari 2025 wamewafikia wananchi zaidi ya 45,000 wakiwemo wanafunzi wa shule mbalimbali.
Masinde amesema TAWA imekuwa ikiwadhibiti wanyamapori hao kwa kutumia nyenzo mbalimbali ikiwemo mabomu baridi waliyopokea kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii hivyo, matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu yameendelea kupungua.
Wananchi wa Kijiji cha Halawa wilayani Bariadi wamepongeza jitihada zinazofanywa na TAWA katika kuwaelimisha masuala mbalimbali ya uhifadhi ikiwemo athari za kuchungia mifugo ndani ya hifadhi na kukiri kuachana nazo kwani zimechangia kupata umasikini hasa pale wanapolazimika kulipia faini mifugo inayokamatwa ndani ya hifadhi.
"Mimi nilikuwa na ng'ombe 30 ambazo nilikuwa nazichungia ndani ya Hifadhi ya Maswa, nilikamatwa na kulazimika kuuza ng'ombe watano ili kulipa faini kuwakomboa, nikabaki na 25. Kwahiyo nilipoteza ng'ombe watano kwa kuchungia hifadhini.
"Sitaki tena kuchungia hifadhini bora nitunze ng'ombe wangu 25 angalau na nyumba nijenge familia yangu ilale pazuri," amesema Ngomanzito Lenhya mkazi wa Kijiji cha Halawa.
