TANZANIA MWENYEJI KONGAMANO LA MAFUTA NA GESI
Na Nora Damian, The Page
Tanzania inatarajia kuwa mweyeji wa kongamano la mafuta na gesi lenye lengo la kujadili kuhusu utafutaji na uendelezaji wa rasilimali hiyo katika nchi za Afrika Mashariki.
Kongamano hilo la 11 na maonesho ya Afrika Mashariki ya mafuta na gesi (EAPCE25) litafanyika Machi 5 hadi 7 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Februari 7,2025 na waandishi wa habari Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema kongamano hilo hufanyika kila baada ya miaka miwili kwa utaratibu wa kupokezana nchi wanachama.
“Kongamano hili limekuja wakati muafaka na litakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkutano wa Nishati Afrika (M300) uliofanyika hivi karibuni hapa nchini kwa sababu litaangalia pia jinsi ya kuendelea kupata nishati ya umeme kutoka vyanzo kama gesi asilia,” amesema Mramba.
Amesema kongamano hilo ambao litafunguliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan litashirikisha washiriki zaidi ya 1,000 ambapo pia kutakuwa na maonesho ya bidhaa na huduma kutoka kwenye kampuni mbalimbali zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi.
“Hii itakuwa ni fursa muhimu kwa wawekezaji wa ndani na nje, wafanyabiashara na wajasiriamali kutangaza bidhaa na huduma zao…ni fursa muhimu ambayo hawapaswi kuiachia,” amesema.
Katibu Mkuu huyo amesema mada mbalimbali zitajadiliwa zinazohusu mafuta na gesi kama vile utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi katika nchi za Afrika Mashariki, fursa za uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi, dhana ya kuelekea kwenye nishati safi ya kupikia, masuala ya mazingira, miundombinu ya kisera, kisheria, kiudhibiti na nyingine
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kikanda ya Maandalizi ya kongamano hilo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio, amesema kongamano hilo ni muhimu kwa sababu linaendeleza uhusiano uliopo katika sekta ya nishati miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kisekta Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jean Havugimana, amesema tangu kuanza kwa makongamano hayo kumekuwa na ushirikiano wa kutosha baina ya nchi za EAC.
Mjiolojia kutoka Wizara ya Nishati na Mafuta Kenya, Josky Kisali, amesema watatumia kongamano hilo kuonesha fursa za uwekezaji zilizopo katika nishati na mafuta kwa kuwa wanatekeleza miradi mbalimbali.
Kaulimbiu ya kongamano hilo ni ‘Kufungua fursa za uwekezaji katika nishati na kuangalia mchango wa rasilimali za mafuta katika kupata nishati ya uhakika kwa maendeleo endelevu ya Afrika Mashariki’.


