KITUO CHA KUPOZA UMEME URAMBO KIMEKAMILIKA - KAPINGA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Uhuru kilichopo Wilaya ya Urambo mkoani Tabora umekamilika.

Kapinga ameyasema hayo leo Februari 7,2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta, aliyetaka kufahamu Serikali itakamilisha lini kituo hicho cha kupoza umeme na lini kitaanza kufanya kazi.

"Ujenzi wa kituo cha kupoza umeme umeshakamilika, hivi sasa kazi inayoendelea ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme, ikikamilika kituo hicho kitaanza kufanya kazi," amesema Kapinga.Akijibu swali la Mbunge wa Nanyumbu, Ally Mhata, aliyetaka kufahamu lini Serikali itashusha bei ya kuunganisha umeme katika Kata za Mangaka na Kilimanihewa kama maombi yalivyowasilishwa wizarani, Kapinga amesema kuna maeneo ya vijiji na vijiji miji ambapo ya vijiji yanaunganishwa kwa Sh 27,000.

Amesema maeneo yenye sura ya Vijiji-Miji yanaunganishwa kwa Sh 320,960 hivyo kwa Kata ya Mangaka na Kilimahewa yenye sura ya Vijiji Miji yanaunganishwa umeme kwa Sh 320,960.

Amesema Serikali inaendelea kuangalia kama kuna uwezekano wa kufanya maboresho ya gharama kutokana na tathmini iliyofanyika.

Kuhusu vitongoji 105 ambavyo havijapata umeme Wilaya ya Nanyumbu, Kapinga amesema hivi sasa Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya kupeleka umeme kwenye vitongoji ikiwemo vitongoji 15 kwa Mbunge na kwa mwaka ujao wa fedha vitaongezwa vingine 38 ili kupunguza idadi ya vitongoji hivyo 105.

Powered by Blogger.