TUGHE, MTANDAO AFYA YA UZAZI WAPONGEZA LIKIZO YA UZAZI KINAMAMA WANAOJIFUNGUA NJITI
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe) kimesema hatua ya Serikali kupitisha Sheria inayoongeza muda wa likizo ya uzazi kwa wanaojifungua watoto njiti itasaidia kulinda ustawi wa watumishi.
Hivi karibuni Bunge lilipitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Kazi namba 13 wa Mwaka 2024, ambapo sasa likizo ya uzazi kwa mwajiriwa ambaye atajifungua mtoto njiti imejumuisha muda uliobaki wa kufikia wiki 40 za ujauzito, huku baba naye akipewa siku saba za kupumzika.
Akizungumza Februari 3,2025 jijini Dar es Salaam Makamu Mwenyekiti wa Tughe, Dk. Jenny Madete, amesema wafanyakazi wanaojifungua watoto njiti wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali hivyo wanahitaji kupata muda wa kupumzika na kumhudumia mtoto hadi wanaporuhusiwa kutoka hospitali.
"Mbali na changamoto za kiafya pia wamekuwa kwenye wasiwasi mkubwa wa kupoteza ajira zao suala linalosababisha kupata msongo wa mawazo na kuathiri malezi ya watoto wanaozaliwa," amesema Dk. Madete.
Mtandao wa Afya ya Uzazi unaoongozwa na Taasisi ya Doris Mollel ambao unajumuisha mashirika zaidi ya 200 ulipaza sauti hatua iliyowezesha kufikia mafanikio hayo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel, Doris Mollel, amesema alianza harakati za kudai nyongeza hiyo ya likizo mwaka 2017 baada ya kukutana na mama ambaye alifukuzwa kazi baada ya kujifungua mtoto njiti na kukaa wodini kwa miezi mitano.
"Nilimuonea huruma changamoto ambazo alikuwa anapitia, wakati nazungumza naye daktari aliniambia kinamama wengi wanaopata changamoto hiyo huwa wanafukuzwa kazi au wanaamua kuchukua likizo bila malipo.
"Gharama za kumlea mtoto njiti ni kubwa kuanzia anapozaliwa, sasa mtu akichukua likizo bila malipo inazidi kuwa changamoto kwake," amesema Mollel.
