RICHARD LYIMO MWENYEKITI TLP TAIFA

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Taifa, Richard Lyimo, akizungumza baada ya kuchaguliwa wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Mkutano Mkuu wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) umemchagua Richard Lyimo kuwa Mwenyekiti wa Taifa huku Johari Hamisi akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Bara na Hamad Mkadam akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar.

Viongozi hao wamechaguliwa Februari 2,2025 wakati wa mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wajumbe 84.

Wengine waliochaguliwa na nafasi zao kwenye mabano ni Yustas Rwamugira (Katibu Mkuu) na Elinihaki Mbwambo (Katibu Mwenezi).

Lyimo ambaye awali alikuwa Katibu Mkuu, amesema ana uzoefu mkubwa kwenye siasa na kuwahakikishia wanachama wa chama hicho kuwa atafanya kazi kwa bidii ili chama kizidi kusonga mbele.

"Kwenye siasa nimeanza na katibu wa tawi, nikawa katibu wa kata baadaye nikawa mwenyekiti wa kata. Nikawa katibu wa jimbo la ubungo baadaye nikawa mwenyekiti wa jimbo.

"Nikawa mwenyekiti wa wilaya, mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam nimefanya kazi nikapandishwa kuwa naibu katibu mkuu, kwahiyo siendi kujifunza najua kwa kuanzia, hakuna hatua ya kisiasa ambayo sijapita...mnaponipa nafasi hii tayari mmewasha mqanga TLP," amesema Lyimo.Naye Makamu Mwenyekiti Bara, Johari Hamisi, amesema atajitahidi kukitengeneza chama hicho kiwe cha kisasa zaidi na kuwahamasisha wanawake kujiunga.

Mkutano huo pia umepitisha azimio la kuwafukuza uanachama wanachama 21 wa chama hicho kwa madai ya uasi.

Wanachama hao wamefukuzwa kufuatia kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanyika Oktoba 8,2024.

Kwa upande wake Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza, amesema mkutano huo ni halali kwa kuwa umefuata taratibu, kanuni, sheria na Katiba ya TLP.

"Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kanuni za usajili na ufuatiliaji shughuli za vyama vya siasa ya mwaka 2019, chama cha siasa kikitaka kufanya mkutano mkuu kinapaswa kutoa taarifa kwa msajili wa vyama vya siasa ili sisi tujiridhishe kama wamefuata utaratibu.

"Tumejiridhisha mkutano unaofanyika leo aliyehitisha ni mtu sahihi kulingana na Katiba ya TLP," amesema Nyahoza.









Powered by Blogger.