TUZO ZA UZALENDO ZAJA, LENGO NI KUHAMASISHA UPENDO

Na Nora Damian, The Page

Taasisi ya Family Vibes imeandaa tuzo maalumu zenye lengo la kukomesha chuki na kuhamasisha upendo kwenye jamii.

Tuzo hizo zijulikanazo kama 'Valentine Eve; Uzalendo Awards' zinatarajiwa kuzinduliwa rasmi Februari 13,2025 jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Akizungumza leo Januari 31,2025 na waandishi wa habari Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk. Maryrose Majinge, amesema chanzo cha chuki ni mmomonyoko wa maadili ambao umesababisha watu kukosa upendo na kutokuwa wazalendo.

"Tutatafakari tiba yake na madhara ya chuki, tutazingatia mchango wa watu mashuhuri katika kukabiliana na mmomonyoko wa maadili na madhara ya chuki."Siku hii ni maalumu kwa ajili ya upendo wa wananchi, utakuwa ni usiku wa uzalendo, kupendana sisi kwa sisi na mazingira yetu...tukipendana sisi hata tukisherehekea Valentine italeta maana," amesema Dk. Majinge ambaye pia ni Daktari wa Maendeleo ya Binadamu na Mbobevu wa Afya Bora ya Akili.

Kwa mujibu wa Dk. Majinge mada mbalimbali kuhusu mmomonyoko wa maadili, masuala ya uchumi na nyingine zitajadiliwa.

Amewataja baadhi ya watu mashuhuri watakaohudhuria tuzo hizo kuwa ni Kamishna wa Maadili, Jaji Sivangilwa Mwangesi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk. Fredrick Shoo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya, Jenister Mhagama na Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo.





Powered by Blogger.