'VYOMBO VYA HABARI VIJISAHIHISHE'
Na Nora Damian, The Page - Dodoma
Matumizi sahihi ya Lugha ya Kiswahili, maudhui yasiyo bora, kukosekana kwa uwiano wa vipindi vya kuelimisha na kuburudisha na kutoripotiwa uchaguzi kwa ukamilifu wake ni kati ya mambo yaliyochomoza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji (ABC).
Mkutano huo ulioanza Februari 13,2025 jijini Dodoma umeandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ukiangazia mwenendo wa sekta ya utangazaji nchini, wajibu wa vyombo vya habari kuelekea Uchaguzi Mkuu, changamoto na suluhu ya kuzikabili.
Akifungua mkutano huo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, ameshauri vyombo vya habari kuacha kudumaza Kiswahili akitahadharisha kuwa suala hilo linaweza kuigharimu Tanzania.
"Tunaanza kuwa na changamoto ya kudumaza Kiswahili, Lugha ya Kiswahili ina utajiri mkubwa wa misamiati na istilahi, lakini tatizo ambalo linaanza kuwa sugu ni kubananga Kiswahili.
"Wabanangaji wakubwa wa Lugha ya Kiswahili ni watangazaji wasiokuwa makini katika matumizi ya lugha kwa mbwembwe na harara ambazo zinaishia kufubaza na kudumaza Kiswahili.
"Vyombo vya habari hasa vya utangazaji vina mchango mkubwa kusahihisha makosa, watangazaji wa redio, televisheni mna jukumu kubwa la kuhakikisha Watanzania wanaongea Kiswahili fasaha na sanifu," amesema Profesa Kabudi.
Waziri huyo pia amesema hakuna uwiano mzuri kati ya vipindi vya kuelimisha, kuburudisha na kuhabarisha na kutolea mfano wa redio kwamba nyingi zimejikita kwenye vipindi vya burudani za muziki na michezo.
Amesema utangazaji ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi katika kuhamasisha amani, mshikamano na ujenzi wa taifa na kwamba utangazaji usiozingatia weledi husababisha mifarakano, machafuko na mauaji.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk. Elisha Magolanga, ambaye aliwasilisha mada kuhusu Rasimu ya Mkakati wa Kukuza Uzalishaji wa Maudhui ya Ndani, amesema sekta ya habari inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kukosa wataalam wenye weledi wa kutengeneza maudhui yenye ushawishi.
"Tunataka tuione 'future' ya Tanzania kwa TV na online TV zikizalisha maudhui yenye ubora wa hali ya juu na yakiwa mengi zaidi," amesema Dk. Magolanga.
Akizungumza kwa niaba ya Watoa Huduma za Maudhui Tanzania, Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Yahya Mohamed, ameshauri uwekwe mkazo wa kuangalia mzizi wa tatizo la maudhui ya ndani.
"Tunaridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali hasa za kuwepo kwa mazungumzo kati ya TCRA na vyombo vya habari.
"Changamoto kubwa ni suala la kisera, kanuni na kuendana na kasi ya teknolojia lakini tunaiona nuru katika siku za usoni ya kuwa na sekta bora zaidi ambayo imeimarika," amesema Mohamed.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir Bakari, amesema wanatumia mkutano huo kutafakari, kubadilishana mawazo na kupeana taarifa zinazohusu sekta ya utangazaji na kutafuta suluhu ya changamoto mbalimbali.
"Sekta ya utangazaji inapitia maboresho makubwa ambayo yanatoa nafasi kwa teknolojia mpya kuingia sokoni na kuleta changamoto mbalimbali zikiwemo za udhibiti.
"Utafiti unaoendelea ukihusisha mshauri mwelekezi wa kimataifa kuhusu mapitio ya mfumo mzima wa usimamizi wa leseni za utangazaji utakuja na majibu sahihi ya kisayansi," amesema Dk. Bakari.
Kulingana na Mkurugenzi huyo utafiti huo ulioanza Aprili 2024 utakamilika Februari 21,2025 unaangazia tathmini ya soko na changamoto za wadau, marejeo ya usimamizi mzima wa leseni za utangazaji na mapitio ya ada za leseni za utangazaji nchini.
Aidha amesema TCRA iko katika hatua za mwisho kukagua takwimu za utangazaji kupitia mifumo ya Tehama ili kufanya tathmini ya mwenendo wa sekta ya utangazaji.
Mkutano huo unaohitimishwa leo pia utafanya tathmini ya utekelezwaji wa maazimio 18 ya mkutano mkuu wa mwaka jana na kutoka na maadhimio ya mwaka huu.



