VITUO VYA UTANGAZAJI VITOE TAARIFA ZA HALI YA HEWA - PROFESA KABUDI
Na Nora Damian, The Page - Dodoma
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amevitaka vituo vya utangazaji nchini kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wananchi na wakulima kuhusu utabiri wa hali ya hewa na athari za tabianchi.
Amesema Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ni miongoni mwa vyombo vya kisasa vya kutabiri mwenendo wa hali ya hewa nchini na duniani hivyo ni muhimu taarifa ziwafikie wananchi waweze kuchukua tahadhari mapema.
Ameyasema hayo Februari 13,2025 jijini Dodoma alipokuwa akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Tanzania (ABC).
Maadhimisho ya mwaka huu yanayongozwa na Kaulimbiu isemayo 'Redio na mabadiliko ya tabianchi; chombo muhimu kwa mabadiliko chanya.
Amesema mabadiliko ya tabianchi ni ajenda muhimu kitaifa na kimataifa ambayo inaathiri maisha ya binadamu siku hadi siku kama vile kuathiri makazi ya watu, uzalishaji wa mazao ya chakula, mabadiliko ya misimu ya mvua na ongezeko la joto duniani.
"Utangazaji kupitia redio umekuwa na nguvu duniani kwa vile matangazo yake hufikia watu wengi kwa haraka na kwa gharama nafuu, wananchi wa hali ya chini, ya kati na ya juu kiuchumi wanaweza kumudu kununua.
"Tuhakikishe tunakuwa na vipindi vya redio vinavyotoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mabadiliko ya tabianchi," amesema Profesa Kabudi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabir Bakari, amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kuzingatia Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu kwa kuhakikisha vinatoa taarifa za utabiri wa hali ya hewa.
Siku ya Redio inalenga kutambua mchango wa redio kama chombo cha kuaminika na chenye gharama nafuu zaidi duniani ambacho hutumika kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii.
