'UTANGAZAJI USIKWAZE UCHAGUZI MKUU'

Na Nora Damian, The Page - Dodoma

Kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, vyombo vya utangazaji vimetakiwa kusimamia haki na usawa katika kuhabarisha taifa mwenendo wa kampeni za vyama vya siasa pamoja na kuzingatia weledi na kanuni za utangazaji.

Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unatarajia kufanyika Oktoba mwaka huu na michakato mbalimbali inaendelea ikiwemo ya kuandikisha wapigakura na kutoa elimu ya uraia kwa wapigakura.

Wito huo umetolewa Februari 13,2025 jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Tanzania (ABC) ulioandaliwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Mkutano huo unaongozwa na Kaulimbiu isemayo 'Wajibu wa Vyombo vya Utangazaji kuelekea Uchaguzi Mkuu' ikikumbusha nafasi ya vyombo vya utangazaji kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba."Washiriki wa mkutano huu hakikisheni mnazielewa sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi mkuu ili wananchi waweze kuridhika na kufanya maamuzi sahihi katika kipindi cha uchaguzi," amesema Profesa Kabudi.

Akiwasilisha mada kuhusu Tathmini ya Chaguzi za Nyuma na Mchango wa Vyombo vya Habari katika Uripoti, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk. Abdallah Katunzi, amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kusimamia masilahi ya umma wakati wa Uchaguzi Mkuu.

"Vyombo vya habari vinatakiwa kuwa gundi inayoleta umoja wa nchi na kukemea kwa nguvu zote wale wanaohatarisha umoja wetu," amesema Dk. Katunzi.

Ameshauri vyombo vya habari kuandaa agenda maalumu za kuripoti uchaguzi, kuandaa vigezo na kuvisimamia, kuwapa watu mafunzo, kuanza kukusanya taarifa muhimu, kujenga utaratibu wa kushirikiana kwa kufanya vipindi vya pamoja na kutafuta rasilimali.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Sheria kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Cyripian amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kuzingatia weledi kwani ndio msingi wa kutoa habari na kufanikisha zoezi hilo muhimu.

"Utoaji habari sahihi zilizofanyiwa utafiti na kuhakikiwa huwezesha uboreshaji kueleweka kwa urahisi. Vyombo vya habari viwe sauti ya kuonesha upotoshwaji wa aina yotote unaofanywa kwa bahati mbaya au kwa makusudi kuhusu tume na zoezi la uboreshaji wa daftari," amesema.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, vituo 40,170 vinatumika kuandikisha wapigakura na kati ya hivyo 39,753 ni vya Tanzania Bara na 417 Zanzibar.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui, Saida Muki, amesisitiza waandishi wa habari kuwa makini na matumizi ya Teknolojia ya Akili Unde (AI) wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu ili kuepuka kuwasilisha maudhui yasiyofaa.










Powered by Blogger.