NAOMI NI MAREHEMU, KIFO CHAKE KILIKUWA CHA MATESO – MAHAKAMA
Na Nora Damian, The Page
Dakika 73 alizotumia Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Hamidu Mwanga kusoma hukumu dhidi ya kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili mfanyabiashara Hamisi Luwonga zimehitimisha kwamba ni kweli alimuua mkewe Naomi Marijani kwa kukusudia na alitumia magunia mawili ya mkaa kumteketeza.
Jaji Mwanga aliyeanza kusoma hukumu hiyo saa 7:06 mchana hadi saa 8:19 mchana alichambua ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo huku pia akitumia mifano ya maamuzi ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama za nje ikiwemo Mahakama ya India.
Mahakama ilijikita kupata majibu katika hoja tatu; kuthibitisha kama Naomi ni marehemu na kifo chake si cha kawaida, kuthibitisha kama Luwonga ndiye alihusika na kifo hicho na kuthibitisha kama alikuwa na dhamira mbovu.
Jaji Mwanga amesema uchambuzi wa kisayansi uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali ulithibitisha kwamba mabaki ya damu, mfupa na jino ni ya mwanamke.
Amesema kesi hiyo ina mazingira tofauti kwa kuwa hakuna mwili uliopatikana wala uchunguzi wa kidaktari uliofanywa lakini yapo maamuzi ya mahakama ambayo yanaonyesha kifo cha mtu kinaweza kuthibitishwa na ushahidi wa kimazingira.
“Maamuzi ya kesi ya Mathias Bundala dhidi ya Jamhuri na Sikujua Idd dhidi ya Jamhuri yanasisitiza kosa la mauaji linaweza kuthibitishwa kwa ushahidi wa mazingira na si lazima ‘postmoterm’ iwe imefanyika au mwili umeonekana.
“Mabaki ya mifupa yaliyokutwa shambani mshtakiwa hakukataa kwamba ilikuwa ya binadamu, alisema kulikuwa na kaburi wakati wanauziwa shamba lakini hakuwahi kuleta ndugu waeleze mahakama walifukuaje kaburi kwa sababu kuna taratibu zake,” amesema Jaji Mwanga.
Hoja nyingine ni kuhusu Mpwa wa mfanyabiashara huyo ambaye alielekezwa na Luwonga kuchimba shimo lililotumika kumchomea Naomi, pia alitumwa kununua magunia mawili ya mkaa na kuelekezwa kuuacha nje ya geti, pia aliona vipande vya nguo kwenye shimo baada ya tukio kutokea.
Kielelezo cha line za simu ya Naomi; baada ya kuchunguzwa ilibainika kuwa meseji hazikutumwa na Naomi bali zilitumwa na mshtakiwa baada ya kutoa line za marehemu na kuweka kwenye simu yake kisha kujitumia meseji zinazoonyesha Naomi amesafiri kwenda nje ya nchi huku zote zikionekana kutumwa eneo moja.
“Wakati wa utetezi mshtakiwa hakukataa kama line alikutwa nazo na kwanini alikuwa nazo wakati sms zilisomeka kwamba Naomi yuko nje ya nchi,” amesema.
Amesema mshtakiwa alidhamiria kusababisha kifo cha marehemu kutokana na vitendo alivyofanya baada ya tukio na maudhui ya ripoti kuhusu afya ya akili yanaonyesha tukio lilifanyika akiwa na akili timamu.
“Baada ya tukio kutendeka alimkunja marehemu kwenye shuka mbili kisha akaupeleka mwili hadi katika banda la kuku alikokuwa amechimba shimo. Akaukalisha kisha akachukua gunia mbili za mkaa na kumchoma, akahakikisha kila kitu kinateketea halafu mabaki akayapeleka shambani kwake kuyafukia…kitendo hiki si cha kibinadamu, alifanya kwa kudhamiria huyu mtu ateketee,” amesema.
Hoja nyingine ni kuhusu maelezo ya onyo ya mshtakiwa na yale aliyoyatoa kwa mlinzi wa amani; Jaji Mwanga amesema yalikubalika bila pingamizi ni ya kweli na yanapaswa kuaminika kwamba ndicho kilichotokea na mshtakiwa ndiye mtu wa mwisho kuonekana na marehemu.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Yasinta Peter na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ashura Mnzava, umedai kuwa kifo cha Naomi kilikuwa cha mateso na ni tukio ambalo liligusa hisia za familia yake na jamii na litamuathiri kisaikolojia mtoto wao.
“Hata kama Naomi alikuwa na mapungufu hakustahili kifo alichokipata, ni cha kinyama, ikifikia hatua ya kuuana ni bora kuachana. Mapenzi hayalazimishwi, mshtakiwa alikuwa na haki ya kuachana naye…suala hili linatupa mashaka hata sisi kina mama wengine na watu wanaotarajia kuingia kwenye ndoa,” amedai Wakili Mnzava.
Upande wa Jamhuri uliiomba mahakama itoe adhabu iwe fundisho kwa wengine na umeiomba mabaki ya mwili wa Naomi yakabidhiwe kwa ndugu zake ili wakafanye mazishi kwa kuwa hakupewa haki ya maziko.
Naye Wakili wa Utetezi, Precious Hassan, amedai kuwa wanakusudia kukata rufaa kutafuta haki zaidi katika mahakama za juu.
Baba mdogo wa Naomi, Robert Marijani, amesema wameridhika na uamuzi uliotolewa na mahakama na kwa sasa wanasubiri wakabidhiwe mabaki ya mwili wa mtoto wao ili wakafanye maziko.
Wakati hukumu hiyo ikisomwa Luwonga ambaye alikuwa amekaa mara zote alionekana akijifuta jasho usoni na kichwani.
Baada ya hukumu kutolewa baadhi ya ndugu zake waliangua vilio akiwemo dada yake ambaye alionekana kuishiwa nguvu hatua iliyolazimu ndugu kumshika hadi nje ya mahakama na kwenda kumpakia kwenye gari ndogo.
Ndugu wa Naomi baada ya kutoka nje ya mahakama walikwenda kukaa katika jengo la kusubiria na kuanza kuangua vilio.
Luwonga alipandishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Julai 30,2019 akikabiliwa na kesi ya mauaji ya mkewe na mara zote alikuwa akisisitiza kwamba amepotea.
Mahakama Kuu imemhukumu kunyongwa hadi kufa.
