POLISI YAKAMATA 26 KWA BIASHARA YA UPATU
Na Nora Damian, The Page
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu 26 kwa tuhuma za kuendesha biashara ya upatu mtandaoni bila kuwa na kibali kutoka Benki Kuu ya Tanzania.
Akizungumza Februari 22,2025 Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Faustine Mafwele, amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kati ya Februari 18 hadi 22 mwaka huu katika maeneo ya Mbagala, Gongolamboto, Tabata, Mbezi Magufuli, Ubungo Riverside na Mabibo.
Amesema watu hao wamekuwa wakifanya shughuli hizo kupitia Kampuni ya LEO BURNETT LONDON (LBL) na kuwahamasisha wananchi kujiunga kwa kulipa Sh 50,000 na kuendelea kwa ahadi kuwa watapata faida kubwa kwa muda mfupi bila ya kuhusishwa kwa namna yoyote katika shughuli za uendeshaji wa kampuni hiyo.
Mmoja wa wananchi waliotapeliwa ambaye pia ni Mchungaji wa Kanisa la EAGT Ulongoni A, John Mwampeli, amesema watu hao walimweleza kwamba wanafanya shughuli hizo kihalali ndipo alipoamua kuweka Sh 540,000 kwa ahadi ya kupata fedha zaidi baada ya mwezi mmoja.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na biashara za upatu mitandaoni bila kujiridhisha kwa kuwa baadhi ya biashara hizo hazina leseni wala vibali kutoka mamlaka za kisheria zinazohusika hivyo kuhatarisha usalama fedha zao.
