WATOTO WALIODAIWA KUIBWA NA DADA WA KAZI WAKUTWA KWA 'SANGOMA'

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro, akizungumza na waandishi wa habari.

Na Nora Damian, The Page

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limefanikiwa kuwapata watoto wawili Husna Gulam (3) na Mahdi Mohamed (4) walioibwa na dada wa kazi kwa kushirikiana na mganga wa kienyeji nyumbani kwao Tandika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Januari 15,2025 na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema watoto hao walipatikana jana.

Amesema watoto hao walipatikana nyumbani kwa mganga huyo Abdulkarim Shariff (43), Kimara Baruti jijini Dar es Salaam ambapo walipelekwa hospitali kufanyiwa vipimo na hawajakutwa na tatizo lolote.

"Mahojiano ya kina na watuhumiwa yanakamilishwa ili kubaini kiini na malengo ya tukio hili, baada ya kukamikisha mahojiano watafikishwa kwenye mamlaka zingine za kisheria kwa hatua zaidi," amesema Kamanda Muliro.

Baba mzazi wa watoto hao Mohamed Kassim, amesema dada huyo wa kazi ambaye bado hajakamatwa, wameishi naye nyumbani kwa siku nne tu, hivyo ilikuwa vigumu kutambua kama anaweza kuwa na dhamira mbaya.

Kamanda Muliro ametoa wito kwa wananchi kuepuka tabia ya kuchukua wasaidizi wa kazi za nyumbani wasiojua historia na tabia zao ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kutokea.


Powered by Blogger.