UMRI WA KUISHI KUFIKIA MIAKA 75 MWAKA 2050
Na Nora Damian, The Page
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema ifikapo mwaka 2050 wanalenga wastani wa umri wa kuishi kwa Mtanzania uwe miaka 75 kutoka 66 ya sasa.
Akizungumza leo Januari 13,2025 wakati wa mkutano wa kuhakiki Rasimu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 kwa kundi la viongozi wa dini amesema kabla watu hawajafariki ni jukumu la Serikali kuweka mazingira mazuri ili waishi muda mrefu wakiwa na afya na furaha.
Amesema mambo makubwa manne wanayoyaona katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni kuwa na taifa jumuishi, taifa lenye ustawi, taifa lenye haki na taifa linalojitegemea.
"Hii ni awamu ya pili ya kukusanya maoni, awamu ya kwanza ilihusisha wananchi na wadau mbalimbali, timu imechakata maoni na kuhusisha vyanzo vingine vya taarifa na kuandaa rasimu ya dira na kuanza awamu ya pili ya kukusanya maoni ya uhakiki.
"Viongozi wa dini ni kundi muhimu linalokusanya jamii kubwa ya Watanzania hivyo, maoni yao ni muhimu kwani yanaakisi maoni ya Watanzania," amesema Profesa Mkumbo.
Aidha amesema kwa miaka 25 iliyopita nchi imekuwa ikitekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ambapo mafanikio mengi yamepatikana na changamoto nyingi zimejitokeza wakati wa utekelezaji wake.
Naye Mkurugenzi wa Programu za Maendeleo na Utetezi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Azgard Stephen, amependekeza dira mpya izingatie umuhimu wa sayansi na teknolojia na mapinduzi ya kidigitali kama kichocheo cha maendeleo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Mohamed Khamis, ametoa wito kwa Tume ya Mipango inayosimamia uandishi wa dira mpya kufanya tathmini kuhusu changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa Dira ya 2025 na kuona namna ya kukabiliana nazo katika dira inayoandaliwa ya 2050.
