COSOTA, TAA ZAINGIA MAKUBALIANO KUKUZA KAZI ZA WASANII
Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) imeingia makubaliano ya ushirikiano na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa lengo la kulipia leseni (mirabaha) kwa matumizi ya muziki katika viwanja vya ndege.
Kupitia makubaliano hayo TAA itahakikisha asilimia 80 ya nyimbo zinazopigwa ni za Tanzania na asilimia 20 ndio za nje ya Tanzania.
Akizungumza leo Januari 13,2025 wakati wa kusaini makubaliano hayo Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema mirabaha ni chanzo muhimu cha mapato kwa wasanii na wanatarajia kuwa hakimiliki ya kazi za sanaa itakuwa na mwelekeo bora na wa haki zaidi.
"Hizi ni jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha sekta ya sanaa na muziki nchini inachagiza maendeleo ya wasanii na kuleta tija.
"Mheshimiwa Rais alionyesha nia ya kuboresha mazingira ya wasanii kwa kutambua mchango wa sanaa katika Taifa letu na umuhimu wa kazi zao na pia kutafuta njia za ziada za kukuza kipato chao pamoja na uchumi wa nchi yetu.
"Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele kusisitiza wasanii kunufaika na kazi zao kwani muziki wa Tanzania unasikika katika maeneo ya umma kama vile viwanja vya ndege hivyo, kuonesha talanta za wasanii na pia kutoa fursa za kibiashara," amesema Mwinjuma.
Naibu Waziri huyo ametoa wito kwa watumiaji wa kazi za wasanii kibiashara kulipia mirabaha kwa wakati na kuongeza ubora katika kufanya kazi zao ili ziwe na tija zaidi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mombokaleo, amesema wamejipanga kutoa ushirikiano kutekeleza makubaliano hayo ili kuhakikisha kuwa wanatekeleza kwa vitendo maelekezo ya Mh Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu kukuza kazi za wasanii wa ndani.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa COSOTA, Doreen Sinare, amesema makubaliano hayo ni ndoto ambayo wamekuwa nayo kwa muda mrefu akisema wameanza na viwanja vya ndege na baadaye watakwenda kwenye maeneo mengine.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ametoa wito kwa wasanii kuendelea kuzalisha kazi zao kwa wingi na kwa ubora unaotakiwa wakizingatia aina na ukubwa wa soko watakalopata kupitia viwanja vya ndege nchini.
