AZAKI ZASISITIZA UCHUMI SHINDANI DIRA YA MAENDELEO 2050
Na Nora Damian, The Page
Asasi za Kiraia (AZAKI) zimehimiza umuhimu wa kukuza uchumi na kuwa shindani ili kutoa hakikisho la ustawi jumuishi na endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Ushauri huo umetolewa Januari 10,2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge, wakati AZAKI zilipokutana kuhakiki Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Kama sekta ya Azaki tunasisitiza sana umuhimu wa kuwa na uchumi shindani, njia bora ya kujua tunafanyaje ni kujilinganisha na wale ambao wametutangulia. Kwahiyo ni muhimu sana kuwa na uchumi ambao ni shindani na lazima ushindani uanzie ndani kwetu sisi wenyewe…tunachotafuta ni ustawi ambao ni jumuishi na endelevu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Rutenge.
Aidha amesema ni muhimu kuwe na chombo kitakachosimamia utekelezaji wa dira hiyo na mifumo ya kufanya tathmini ya utekelezaji huku akipendekeza Azaki zitumiwe kwa kuwa zina utaalam mkubwa katika eneo hilo.
Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni nzuri na wanaamini itawezesha kufikia malengo ya maendeleo na kuahidi kushirikiana na Serikali na wadau wadau wengine katika kuhakikisha eneo hilo linatekelezwa kikamilifu na kuleta matokeo chanya kwa wananchi wote.
Azaki pia zimependekeza suala la utawala na uongozi bora kuwekwa kama sekta muhimu za kimageuzi kwa sababu unahitajika uongozi bora na siasa safi kuwezesha kufikia maendeleo tunayoyataka.
“Sekta ya elimu haijawekwa kama moja ya sekta ya kimageuzi, ili kuhakikisha dhana ya teknolojia inaendelea kuwa thabiti, elimu ni nyenzo kuu katika kuhakikisha kwamba teknolojia inarithishwa kwenye kizazi chetu na kuleta tija katika uzalishaji,” amesema.
Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, amezishukuru Azaki kwa michango yao katika dira hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi maoni waliyoyatoa.
“Asasi za kiraia ni muhimu sana katika kukuza demokrasia, maendeleo endelevu na usalama, Azaki zinachochea ushiriki wa wananchi katika masuala ya kisiasa na kijamii, zinatoa huduma kama vile elimu, afya na msaada kwa makundi yaliyokandamizwa. Zinatetea haki za mazingira, kusaidia katika utawala bora kwa kusimamia uwazi na uwajibikaji wa Serikali kwa kufanya utafiti ili kubaini changamoto na kutoa suluhu,” amesema Nyongo.
