LALJI FOUNDATION YASAIDIA SARE ZA SHULE KWA WATOTO YATIMA 400

Watoto yatima kutoka katiķa vituo mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Taasisi ya Lalji baada ya kukabidhiwa msaada wa sare za shule, Dar es Salaam.


Na Nora Damian, The Page

Watoto yatima 400 kutoka katika vituo tisa vya makao ya kulelea watoto jijini Dar es Salaam wamepatiwa msaada wa sare za shule ili kuwawezesha kutimiza ndoto zao. 

Msaada huo unaojumuisha sare za shule, viatu na mabegi ya kubebea madaftari umetolewa na Taasisi isiyokuwa ya kiserikali inayojihusisha na masuala mbalimbali ya kijamii ya Lalji Foundation.

Akizungumza leo Januari 9,2025 wakati wa kukabidhi misaada hiyo, Mwenyekiti wa Lalji Foundation, Imtiaz Lalji, amesema lengo la kutoa misaada hiyo ni kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma katika kupata elimu. “Tangu mwanzo tumekuwa tukiamini kwamba shughuli zote anazotujalia Mwenyezi Mungu siyo kwa nguvu zetu bali tunapaswa pia kugawa kwa wahitaji kwa sababu furaha kubwa inapatikana kwa kuwahudumia wengine hasa wanaohitaji msaada…tunaamini kila tendo la huruma linachangia kuacha urithi wa kudumu na maono mema kwa vizazi vijavyo,” amesema Imtiaz. 

Aidha ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri yanayowezesha mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kufanya kazi zake kwa amani na kutimiza malengo waliyokusudia.

Naye Katibu wa taasisi hiyo, Fatema Lalji, amesema ilianzishwa mwaka 2022 ikilenga kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo yatima kwa kuwanufaisha kiuchumi, kielimu na kijamii.“Tunaamini ukimsaidia mtu mmoja anabadilisha maisha yake na kusaidia watu wengine, kwahiyo tutaendelea kusaidia watoto yatima na huu utakuwa ni mradi endelevu,” amesema Fatema. 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ally Khamis, ambaye alikuwa mgeni rasmi ameipongeza taasisi hiyo kwa kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya elimu.

Aidha amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha watoto wote wanalindwa na kupata haki zao na kuwaasa watoto waliopata msaada huo kuzingatia masomo na kujiepusha na mambo yasiyofaa. 




Powered by Blogger.