TRAFIKI WAWILI WAKAMATWA DAR KWA TUHUMA.ZA RUSHWA
Na Nora Damian, The Page
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata askari wawili wa usalama barabarani walioonekana kwenye video iliyosambaa mitandaoni wakifanya vitendo visivyo na maadili vya kuchafua taswira ya jeshi hilo.
Akizungumza leo Januari 15,2025 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema askari hao Koplo John na WP Koplo Mgisi, kwa sasa wapo mahabusu na tayari hatua za kinidhamu za mashtaka ya kijeshi zimeanza, huku wakisubiri hatua nyingine za kisheria.
Video hiyo iliyosambaa mitandaoni inawaonesha askari hao wakichukua rushwa kwa madereva wa magari madogo na mabasi ya abiria.
Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vyovyote vya kulidhalilisha vilivyo kinyume na maadili ya jeshi au kuchafua taswira ya Serikali.
