PUGU MARATHON 2025 KUENDELEZA MATENDO YA HURUMA
Na Nora Damian, The Page
Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam limezindua msimu wa tatu wa mbio za hisani (Pugu Marathon) zinazolenga kufanya matendo ya huruma kwa jamii.
Akizungumza leo Januari 21,2025 jijini Dar es Salaam Askofu Msaidizi Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Stephano Musomba, amesema mbio hizo pia zitahusisha utoaji huduma za afya bure na kuwataka wananchi kujitokeza kupima afya zao na kujitolea damu kusaidia wagonjwa wenye uhitaji.
"Malengo ya Pugu Marathon msimu wa tatu ni kuendeleza Kituo cha Hija Pugu, kuendeleza Shule ya Sekondari Pugu kwa kuboresha maktaba na nyumba aliyoishi Hayati Mwalimu Julius Nyerere na kufanya matendo ya huruma katika hospitali za Dar es Salaam na kujenga afya kupitia michezo," amesema Askofu Musomba.
Amesema msimu wa pili wa 2024 walikusanya Sh milioni 160 kutoka kwa wakimbiaji na wafadhili mbalimbali ambazo zimeelekezwa katika maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa askofu huyo, Sh milioni 2 zitatumika kununua vitabu kwa ajili ya Shule ya Sekondari Pugu, Sh milioni 3 zitatolewa katika Kituo cha Afya Pugu Kajiungeni kununua mashuka na Sh milioni 10 zitapelekwa kuendeleza Kituo cha Hija Pugu.
Amewataka waumini wa jimbo hilo kujitokeza na kujisajili kwa ajili ya kushiriki katika mbio hizo.
Mbio hizo za Pugu Marathon zilianza rasmi mwaka 2023 na kwa mwaka huu zinatarajiwa kufanyika Mei 31,2025 katika viwanja vya Hija Pugu zikiwa na umbali wa kilomita 2.5, kilomita 5, kilomita 10 na kilomita 21.
