TMA YATOA ANGALIZO MVUA ZA MASIKA
Na Nora Damian, The Page
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imezitaka mamlaka za maafa nchini kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua za masika.
Hayo yamesemwa leo Januari 23,2025 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk. Ladislaus Chang'a, wakati akitoa taarifa ya uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za Masika zinazotarajiwa kuanza Machi hadi Mei mwaka huu.
Amesema vipindi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, hivyo kusababisha uharibifu wa miundombinu, mazingira, mlipuko wa magonjwa pamoja na upotevu wa mali na maisha.
"Mamlaka husika katika Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini inashauriwa kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
"Wasimamizi wa shughuli za mazingira wanashauriwa kuzingatia taarifa hii ipasavyo. Mamlaka husika na Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi za mikoa, wilaya, kata na vijiji/mitaa zinashauriwa kuchukua hatua stahiki ikiwemo kutoa elimu ya maafa na miongozo itakayohamasisha katika kujiandaa, kuzuia au kupunguza na kukabiliana na maafa pamoja na kuhamasisha uhifadhi wa chakula," amesema Chang'a.
Kaimu Mkurugenzi huyo amesema mvua za masika zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Machi katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria na Pwani ya Kaskazini na katika wiki ya pili na ya tatu ya Machi katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki.
Aidha amesema ongezeko la mvua linatarajiwa kuwepo Aprili.
"Vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
"Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka hivyo kuongeza hatari ya mafuriko hususan katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko," amesema.
Msimu wa mvua za masika ni mahususi kwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), Pwani ya Kaskazini (Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, Mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba), Ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
