NECTA YAFUTA MATOKEO YA WATAHINIWA 67

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Said Mohamed, akitangaza matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne, Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limefuta matokeo yote ya watahiniwa 67 waliobainika kufanya udanganyifu na watano walioandika lugha ya matusi katika Mtihani wa Kidato cha Nne uliofanyika Novemba mwaka jana.

Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 (2) (1) cha Sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 30(2) (b) cha Kanuni za Mitihani Mwaka 2016.

Uamuzi huo umetangazwa leo Januari 23,2025 jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed, wakati akitangaza matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne.

"Baraza la Mitihani limekifungia kituo cha BSL Open School kilichopo Mkoa wa Shinyanga kuwa kituo cha Mitihani ya Taifa kutokana na kuratibu mipango ya udanganyifu," amesema Dk. Mohamed. 

Aidha amesema baraza limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 459 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani huo kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo.

Amesema watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakuyafanya kwa sababu ya ugonjwa mwaka huu.

Kuhusu ubora wa ufaulu amesema kwa Madaraja ya I - III ni mzuri zaidi kwa wavulana ikilinganishwa na wasichana.

Kulingana na Katibu hiyo, wavulana ni 119,869 sawa na asilimia 48.90 ya wavulana wote wenye matokeo na wasichana ni 102,084 sawa na asilimia 37.59 ya wasichana wote wenye matokeo. 

"Watahiniwa wengi wamefaulu somo la Kiswahili ambao ni asilimia 97.43. Mathematics lina ufaulu ulio chini ya wastani ambao ni asilimia 25.35, ufaulu wa somo la Basic Mathematics umeshuka kidogo kwa asilimia 0.07 na katika somo la Additional Mathematics umeshuka kwa asilimia 2.70 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2023," amesema Dk. Mohamed.

Kati ya watahiniwa 529,329 wa Shule waliosajiliwa, watahiniwa 517,460 sawa na asilimia 97.76 walifanya mtihani ambapo wasichana walikuwa 271,918 sawa na asilimia 97.54 ya wasichana wote huku wavulana wakiwa 245,542 sawa na asilimia 98.00 ya wavulana wote. Watahiniwa 11,869 sawa na asilimia 2.24 hawakufanya mtihani.




Powered by Blogger.