KISHINDO CHA RAIS SAMIA SEKTA YA UTALII CHASIKIKA KILWA

Na Beatus Maganja, Kilwa

Kazi kubwa ya kutangaza vivutio vya utalii iliyofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inaendelea kudhihirika na kishindo chake kutikisa katika Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia ya Magofu ya Kale ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara kupokea makundi ya watalii wa nje kutoka mataifa mbalimbali.

Hifadhi hiyo iliyo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imefungua ukurasa mpya wa mwaka 2025 Kwa kupokea watalii wa kigeni.

Januari 18, 2025 ilipokea wageni 98 na Januari 22, 2025 imepokea watalii wapatao 173 kutoka Mataifa ya Uingereza, Finland, Sychelles, Marekani, Sweden, Australia na Ireland ambao kwa kutumia meli ya Hebridean Sky walifika hifadhini humo Kwa lengo la kutalii.Hatua iliyochukuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kucheza filamu ya Royal Tour iliyokuwa na lengo la kuhuisha Sekta ya Utalii nchini kutokana na kufifishwa na janga la UVIKO 19, imesaidia kuchechemua sekta ya utalii na kuifanya TAWA kupata idadi kubwa ya wageni wanaotembelea katika maeneo inayosimamia kwa shughuli za utalii wa picha na uwindaji wa kitalii.

Katika kipindi cha mwaka 2023/24 TAWA kupitia Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ilipokea meli 9 za kitalii na jumla ya watalii wa Kigeni 1,047.



Powered by Blogger.