MASHINDANO YA KUHIFADHI QURAN KUFANYIKA FEBRUARI 23, SAMIA MGENI RASMI

Na Nora Damian, The Page

Mashindano ya kimataifa ya Quran Tukufu yanatarajiwa kufanyika Februari 23 mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Januari 30,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mashindano ya mwaka huu, Mwenyekiti wa Tuzo ya Kimataifa Quran Tukufu Tanzania, Sheikh Othman Kaporo, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ndiye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo.

Amesema mashindano hayo yatahudhuriwa na wageni mbalimbali akiwemo Imamu wa misikiti mojawapo mitakatifu ya Kiislamu huko Macca na Madina.

Amesema ujio wa Imamu huyo na wageni wengine mashuhuri unatokana na heshima kubwa ambayo Tanzania imejijengea katika uandaaji wa mashindano hayo.

"Kutakuwa na zawadi kwa washindani 25 watakaoshiriki na Mfalme wa Saudi Arabia naye ametoa ofa kugharamia safari ya kwenda kuhiji miongoni mwa wale watakaofika uwanjani," amesema Sheikh Kaporo.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amepongeza waabdaaji wa tuzo hizo kwa kusisitiza juu ya umuhimu wa kulinda amani.

"Quran na amani vinaenda sambamba na Watanzania wote tunajivunia amani. Wakati wote hatutachoka kuwaunga mkono," amesema Ulega.Uzinduzi huo pia umehudhuriwa na Balozi wa Saudi Arabia nchini, Sheikh Yahya bin Ahmad Okeish.



Powered by Blogger.