DK. MPANGO AHIMIZA MIKAKATI KUKABILI MABADILIKO YA TABIANCHI
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango amehimiza juhudi za kitaifa katika kuimarisha mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza leo Januari 29,2025 katika Kongamano la Nne la Kisayansi la Maji lililoandaliwa na Chuo cha Maji, amesisitiza umuhimu wa tafiti na uvumbuzi katika kukabiliana na changamoto za sekta ya maji.
"Mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuathiri utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, hususan lengo namba sita linalohusu maji na usafi wa mazingira.
"Ukame na mafuriko yanayosababishwa na mabadiliko haya siyo tu yanapoteza maisha ya wananchi wetu, bali pia yanaharibu miundombinu na kusababisha upungufu wa chakula," amesema Dk. Mpango.
Amesema rasilimali maji ina umuhimu mkubwa kufikia Malengo ya Maendelo Endelevu lakini mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa inayoweza kusababisha kutofikiwa kwa lengo hilo.
Amehimiza Chuo cha Maji kuwekeza zaidi katika kubadilishana uzoefu na kufanya tafiti zitakazoleta jawabu la athari za mabadiliko ya tabianchi, changamoto za maji na uondoaji wa majitaka, usalama na uendelevu wa rasilimali za maji, matumizi ya taka ngumu na usimamizi wa vyanzo vya maji pamoja na kuzalisha wahitimu wenye ujuzi wa kukabiliana na changamoto hizo.
"Tunapaswa kutumia fursa hii kuandaa wataalamu wa sekta ya maji ambao watakuwa na uelewa wa kina wa changamoto za kisekta na namna ya kupambana nazo," amesema.
Dk. Mpango amekipongeza Chuo cha Maji kwa kuanzisha Jarida la 'Journal for Water Engineering Management and Policy' akisisitiza kuwa linapaswa kuwa chombo cha kutoa tafiti zenye manufaa kwa watunga sera na watoa maamuzi.
"Tunahitaji tafiti zenye ushahidi wa kisayansi zitakazosaidia kuboresha sera zetu za maji. Tafiti hizi lazima ziwe na takwimu sahihi na mapendekezo yanayoweza kufanyiwa kazi," amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza katika kuboresha miundombinu ya Chuo cha Maji ili kuzalisha wataalam bora wa sekta hiyo.
"Zaidi ya watumishi 9,200 wa sekta ya maji nchini wamepitia katika chuo hiki. Ni lazima tuendelee kuwajengea uwezo kupitia mafunzo ya muda mrefu na mfupi, warsha, na makongamano kama haya," amesema Waziri Aweso.
Aidha amesema Wizara ya Maji imeanzisha Kampuni ya Ushauri ya Water Institute Consultancy Bureau Limited ili kutumia wataalamu waliostaafu kuwajengea uwezo vijana wanaoingia katika Sekta ya Maji.
"Tunataka kuona Chuo cha Maji kikizalisha wataalam mahiri, wachapakazi na wenye uwezo wa kufanya tafiti za kina zinazoweza kutatua changamoto za maji na usafi wa mazingira nchini," amesema.
Kongamano hilo linalenga kuendeleza tafiti na miradi bunifu itakayosaidia sekta ya maji kuwa na ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na changamoto zote za kisekta.
Chuo cha Maji kimeazimia kuendelea kuboresha mitaala yake na kushirikiana na wadau wa sekta ya maji ili kuhakikisha ufanisi wa sekta hiyo nchini Tanzania.
