WAFANYABIASHARA 1,520 KUREJESHWA SOKO LA KARIAKOO

Na Nora Damian, The Page

Wafanyabiashara1,520 wanatarajiwa kurejeshwa katika Soko la Kariakoo kuanzia mwezi ujao baada ya kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa soko hilo.

Idadi hiyo imepatikana baada ya uhakiki wa wafanyabiashara ulifanywa na timu maalumu iliyoundwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ikijumuisha wawakilishi wa wafanyabiashara, menejimenti ya Shirika la Masoko ya Kariakoo na vyomba vya usalama.

Akizungumza leo Januari 29,2025 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Bodi ya Soko la Kariakoo, Hawa Ghasia,  amesema kati ya wafanyabiashara hao 366 wana madeni ambapo wanadaiwa Sh milioni 358.5 hivyo wanatakiwa kuyalipa kabla ya kurejea sokoni.

"Menejimenti inaratibu kazi ya kutangaza majina ya waliokuwa wafanyabiashara kwenye soko hilo ambao wamekidhi vigezo na sifa za kurejeshwa baada ya uhakiki," amesema Ghasia. 

Amesema wafanyabiashara na wananchi wote wenye sifa za kuingia sokoni watatangaziwa utaratibu utakaotumika na kuwataka kuendelea kuwa na subira wakati mamlaka zikikamilisha taratibu. 

Soko la Kariakoo liliungua moto Julai 10 mwaka 2021 na kusababisha wafanyabiashara kuondolewa na shughuli kusimama ambapo ujenzi na ukarabati ulianza Januari 2022 na kugharimu Sh bilioni 28.03.




Powered by Blogger.