DK. ABBASI AITAKA SEKTA BINAFSI KUSHIRIKIANA NA WIZARA KUTANGAZA UTALII
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi ametoa wito kwa sekta binafsi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutangaza mazuri yatokanayo na utalii sehemu mbalimbali za dunia.
Dk. Abbasi ameyasema hayo Januari 29,2025, alipokuwa katika mazungumzo na vyama mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini katika kikao kilichofanyika Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kimelenga kujadiliana masuala mbalimbali ya kuboresha shughuli za utalii, kusikiliza changamoto na kuzitolea majibu.
Akizungumza wakati wa kikao hiko Dk. Abbasi amesisitiza wadau kuendelea kusema mazuri ya sekta ya utalii yaliyofanyika kwa kuwa hakuna sehemu yenye mafanikio isiyo na changamoto.
"Kila mmoja awe balozi wa utalii, semea mazuri ya sekta yetu ya utalii na tuendelee kuupigania utalii wetu kila mmoja kwa wakati wake," amesisitiza Dk. Abbasi.
Amesema Wizara ya Maliasili imepokea maoni na ushauri uliotolewa na wadau wake na kwamba itaendelea kushirikisha wadau kwenye masuala mbalimbali ili kuendelea kuboresha mazingira yao ya kazi na kuhakikisha utalii unazidi kukua zaidi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), Henry Kimambo, amesema changamoto waliyonayo ni kuhusu tangazo lililotolewa hivi karibuni kuhusu mabadiliko ya tozo mpya za Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu pamoja na Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori (WMA).
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mlage Kabange, amesema maboresho ya tozo hizo mpya yalishirikisha wadau.
Amesema maboresho yalifanyika kwa kuzingatia masuala mbalimbali yakiwemo kuimarisha shughuli za uhifadhi katika maeneo hayo sambamba na kuboresha miundombinu ya hifadhi.
Vilevile Kamishna Kabange amesema TAWA itaendelea kukaa na wadau na kujadiliana maeneo yenye changamoto katika kanuni hizo na kukubaliana jinsi ya kuboresha.
Kikao hicho kiliwakutanisha maofisa waandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Kwa upande wa wadau wa utalii Tanzania Association of Tour Operators (TATO), Tanzania Hunting Operators Association ( TAHOA), Tanzania Local Tour Operator (TLTO), Tourism Confederation of Tanzania of Tanzania (TCT), Hotel Association of Tanzania (HAT) walishiriki.


