MAAMBUKIZI MINYOO YA TUMBO, KICHOCHO YAPUNGUA

Waziri wa Afya, Jenister Mhagama, akizungumza kuhusu maadhimisho ya siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, Dar es Salaam.

Na Nora Damian, The Page

Serikali imesema juhudi za kuyadhibiti magonjwa ya minyoo ya tumbo na kichocho zinaendelea katika Halmashauri zote 184 huku takwimu za wagonjwa wanaoripotiwa zikiashiria maambukizi katika ngazi ya jamii yamepungua. 

Kauli hiyo imetolewa leo Januari 29,2025 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Jenister Mhagama, alipokuwa akizungumzia maadhimisho ya siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele.

Waziri Mhagama amesema hadi kufikia Desemba mwaka jana watoto 8,676,234 wenye umri wa miaka 5-14 walipatiwa huduma ya kingatiba kwa ugonjwa wa minyoo ya tumbo.

Amesema kwa ugonjwa wa kichocho watoto 6,289,884 kutoka katika halmashauri 171 walimeza kingatiba za kudhibiti ugonjwa wa kichocho."Wizara kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele inadhibiti magonjwa matano ambayo ni Matende na Mabusha (Ngirimaji), Trakoma (Vikope), Usubi, Kichocho, na Minyoo ya Tumbo.

"Udhibiti huo unafanywa kupitia ugawaji wa kingatiba kwa walengwa mbalimbali walio katika mazingira hatarishi dhidi ya magonjwa haya.

"Magonjwa haya matano pamoja na kusababisha usumbufu mkubwa kwa waathirika, pia yanaongeza matumizi ya rasilimali chache tulizonazo katika kuyakabili," amesema Waziri Mhagama.

Aidha amesema kwa mwaka 2024 watu 7,323,634 walipatiwa kingatiba za kutokomeza ugonjwa wa matende na mabusha, usubi na trakoma.

Amezitaja njia za kutokomeza magonjwa hayo kuwa ni pamoja na kushiriki katika kampeni za kumeza kingatiba kila mwaka na kufuata kanuni za afya ikiwa ni kuzingatia usafi wa mazingira, usafi binafsi, kubadili tabia hatarishi, kunawa mikono kila wakati na kutumia vyoo bora.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema 'Tuungane, Tuchukue hatua, Tutokomeze Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele'.









Powered by Blogger.