BIASHARA KARIAKOO SAA 24 KWA WIKI
Na Nora Damian, The Page
Kufuatia kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa Soko la Kariakoo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema biashara zitafanyika kwa saa 24 ili kukuza uchumi wa wafanyabiashara na mkoa huo.
Akizungumza leo Januari 30,2025 wakati akitangaza uamuzi huo, amesema uzinduzi rasmi utafanywa Februari 22,2025.
"Ujenzi na ukarabati umekamilika kwa asilimia 97, zimebaki kazi ndogondogo zinaendelea kama za kufunga taa. Niwaombe wafanyabiashara kutumia fursa hii kufanya biashara zenye viwango na zinazokidhi vigezo vya kimataifa," amesema Chalamila.
Katika hatua nyingine amesema kamati maalumu itaundwa na kupitia majengo yote yaliyochakaa katikati ya mji na yasiyo akisi sura ya mji ili kupata wabia wa kuongeza hoteli za kitalii na kumbi za mikutano.
Kuhusu wafanyabiashara wa soko hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Masoko Kariakoo, Hawa Ghasia, amesema kuanzia kesho wataanza kutangaza majina ya wafanyabiashara waliokuwepo kabla soko halijaungua kisha watatoa fursa kwa wafanyabiashara wengine kuomba nafasi.
